June 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KMC yahamishia hasira kwa Maafande

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

KIKOSI cha timu ya KMC tayari kimeshawasili jijini Dodoma na kuanza mazoezi huku wakiwatangazia kichapo wenyeji wao JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) utakaochezwa Desemba 23 katika uwanja wa Jamhuri.

KMC wamewafuata wapinzani wao huku wakiwa na hasira ya kupokea kichapo cha goli 1-0 kutoka kwa Ihefu katika mchezo wao wao juzi uliochezwa kwenye uwanja wa Highland Estates.

Matokeo hayo waliwashusha KMC kutoka nafasi ya tano hadi ya nane katika msimamo wa Ligi na sasa wanahaha kushinda mchezo huo ili kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi wakiwa katika nafasi za juu.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwagala ameuambia Mtandao huu kuwa, kwa sasa benchi lao la ufundi limeweka mikakati imara itakayowawezesha kurudi kwenye ubora wao kwani wamebaini mapungufu yaliyowafanya kupoteza mechi tatu mfululizo tena zote za ugenini dhidi ya Mtibwa, Sugar, Simba pamoja na Ihefu.

Amesema, bado hawajavunjika moyo na wanazidi kuwa imara kwani wanaamini wachezaji wao wataingia uwanjani na morali ya hali ya juu jambo litakalowawezesha kupata alama tatu ugenini ambazo zitawarudisha kwenye nafasi yao.

Pia amesema kuwa, bado wanaimani kubwa sana na wachezaji wao ambao wamekuwa wakipambana na kuonesha kiwango bora kwa dakika zote 90, hivyo kikubwa ni mashabiki kuwaongezea morali ili kutimiza wanachokihitaji.

“Licha ya kupoteza mechi tatu mfululizo lakini si viongozi wa benchi la ufundi wala wachezaji waliovunjika moyo bali ndo yametuoingezea morali ya kupambana zaidi kwani hatutaruhusu kupoteza alama nyingine tatu muhimu ambazo zitaturudhisha kwenye mstari. Kikubwa ni mashabiki kuendelea kutusapoti ili tuweze kufanikisha kupata kile tunachokihitaji,” amesema Mwagala.