November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Profesa Kitila Mkumbo, mgombea Ubunge Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CCM

Kitila akubali ulezi timu za Ubungo

Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekubali ombi la kuwa Mlezi wa vilabu vya Soka vya jimbo hilo, endapo atachaguliwa kuwa mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Akizungumza katika Uwanja wa Kinesi jijini Dar es Salaam jana, Kitila amesema amepokea maombi mengi ya kumtaka awe mlezi wa timu za jimbo hilo, jambo alilosema ni la heshima kubwa kwake.

Kwa mara ya kwanza Kitila alipewa ombi la kuwa mlezi wakati alipotembelea katika ofisi za klabu maarufu ya Friends Rangers iliyopo eneo la Magomeni Kagera ambako alielezwa chanzo kikubwa cha Ubungo kukosa timu Ligi Kuu ni ukosefu wa kiongozi mlezi wa kuviangalia vilabu hivyo.

“Nimepokea kwa mikono miwili ombi la vilabu vya Manzese kunitaka niwe mlezi wao endapo nitashinda kuwa mbunge. Hii ni heshima kubwa kwangu na nawaahidi kwamba nikishinda huu mchaguzi, nitalibeba jukumu hilo kwa heshima kubwa, alisema Profesa Mkumbo.

Kitila alikwenda kwenye uwanja huo wa Kinesi kujitambulisha kwa viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ubungo, waliokuwa wamekutana kwa ajili kujadili maandalizi ya mashindano ya Ligi Daraja la Tatu ngazi ya Wilaya.

Kwa upande wake, mwakilishi wa vilabu vya Ubungo, Amour Amour, alimwambia mgombea ubunge huyo kwamba ni jambo linalowaumiza kwamba vilabu vya jimbo hilo na Kibamba vinapata shida kwa mambo ambayo utatuzi wake unahitaji busara tu za viongozi.

“Kuna mambo kama ya viwanja vya soka. Kuna viwanja ambavyo vinatakiwa kuwa vya Ubungo lakini tunanyimwa kwa sababu ambazo hazieweki. Kuna timu zetu zinafanya vibaya kwenye mashindano kwa sababu tu hatuna baba wa kulelea timu hizo. Kwenye wilaya nyingine wanapata msaada lakini hapa hawapati,” amesema kiongozi huyo.

Kiongozi huyo alizungumza kwa uchungu kuhusu namna timu za Ubungo zisizo na mfadhili wala mlezi, zinavyopata taabu kwa kupangiwa kwenda mikoa ya mbali kushiriki mashindano ya ligi za kitaifa – jambo linalozinyima uwezo wa kufanya vizuri.

Zaidi ya kuzungumzia suala la ulezi wa vilabu vya soka, Kitila pia ametembelea pia kambi za mazoezi kwa wachezaji wa mchezo wa ngumi; ambao ni mmoja wa michezo inayopendwa zaidi Ubungo.