June 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi wa Mwenge apongeza wananchi kupelekewa huduma ya maji Handeni

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Handeni

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi amesema ushirikiano uliopo kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, umesaidia kuondoa adha ya maji kwa wananchi wa Kijiji cha Kwedizinga, Kata ya Kwedizinga, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Ameyasema hayo Juni 6, 2025 alipofika kuweka Jiwe la Ufunguzi wa Mradi wa Maji Kwedizinga, na kuongeza kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo, na utawasaidia kwa kiwango kikubwa kuondokana na shida ya maji, huku akiwamwagia sifa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga.

“Kutokana na maendeleo ya nchi yetu, Serikali inahakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Wakati tunakuja hapa, Mkuu wa Wilaya (ya Handeni) alikuwa ananieleza kwamba, eneo tunalokwenda tutakuta mradi wa maji safi na salama. Wananchi wetu walikuwa wanapata shida sana ya maji kwenye maeneo hayo, lakini leo hii kwa mapenzi ya Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan), lakini na mapenzi ya uongozi wa wilaya na Kamati ya Ulinzi na Usalama, tunawashukuru kwa usimamizi wa mradi huu.

“Lakini pia niwaombe watu wa RUWASA, leo hii tumekuja kujionea hapa mradi huu umekwenda kuleta hamasa kubwa kwa wananchi, lakini pia umekwenda kuleta imani juu ya Serikali ya Awamu ya Sita. Kwa kweli wana RUWASA wakiongozwa na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga (Mhandisi Upendo Lugongo) tunawashukuru, na hongereni kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa wananchi hawa” alisema Ussi.

Ussi pia, aliwashukuru Wahisani wa maendeleo, Shirika la World Vision Tanzania na We are Water Foundation ya Uhispania kwa kuchangia sehemu kubwa ya ujenzi wa mradi huo.

Akisoma taarifa hiyo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Handeni Mhandisi Hosea Mwingizi, alisema Mradi wa Maji Kwedizinga umetekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la World Vision Tanzania ambalo liliingia Mkataba na kampuni ya ujenzi ya Arusha Drilling Company, Engineering Plus Company Ltd, Viva Top Wonders Company kujenga miundombinu ya kusambaza maji Kwedizinga. 

Mhandisi Mwingizi alisema, mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili 5, 2024 na kukamilika mnamo Aprili 30, 2025. Gharama ya mradi ni 269,458,356 pamoja na kodi kutoka kwa Wahisani, ambapo hadi kufikia hatua ya ukamilishwaji wa mradi fedha zote zimetumika kwa kazi za uchimbaji wa kisima mita 111 kinachozalisha lita 15,840 kwa saa, ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji, ujenzi wa tenki la maji ujazo wa lita 50,000 ujenzi wa nyumba ya mtambo, ufungaji mfumo wa umeme wa solar, uchimbaji na ulazaji bomba kilomita 8.5 ikihusisha nguvu ya wananchi kwa sehemu (uchimbaji mtalo jumla ya mita 600) sawa na shi. milioni 1.8, na World Vision Tanzania alitoa sh. 267,658,356.

“Manufaa ya mradi huu ni upatikanaji wa uhakika wa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 3,330 kwa kuongeza muda wa uzalishaji mali kwa wananchi ili kukuza uchumi wa nchi, kuondoa athari ya milipuko ya magonjwa. Mradi huu umekabidhiwa Ofisi ya RUWASA Handeni na kwa sasa unaendeshwa na Chombo cha Maji Kwamgwe chenye Usajili Na.R-TNG-HD-003.

“Shukrani zimwendee Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha mahusiano mazuri na wadau wa maendeleo katika kuchangia jitihada za  Serikali kumtua mama ndoo kichwani ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi wa Mwaka 2020.
Wananchi wa Handeni tunaunga mkono kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2025 inayosema “Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu, wa mwaka 2025, kwa Amani na utulivu”. Pia tunaendelea kutoa elimu pamoja na kutunza mazingira, aidha tupo tayari kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa kuwa ni haki yetu” alisema Mhandisi Mwingizi.