November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi mbio za Mwenge ataka Wizara ya Maji kutoa fedha mradi ukamilike

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Handeni

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava ametaka apewe nakala ya barua ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) kwenda kwa Wizara ya Maji, ikiomba fedha ili kukamilisha mradi wa maji Kwediyamba uliopo Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga.

Lengo la kutaka nakala ya barua hiyo ni kumkumbusha Waziri wa Maji Jumaa Aweso ili aweze kutoa fedha zilizobaki kiasi cha milioni 478.6 ili kukamilisha mradi huo na wananchi wapate maji safi na salama.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akiweka Jiwe la Msingi mradi wa maji Kwediyamba,kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili, Albert Msando

Ameyasema hayo Aprili 19, 2024 wakati alipofika kukagua pamoja na kuweka jiwe la msingi katika mradi huo na kuongeza kuwa Serikali kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo ni kutaka ukamilike, na wananchi wanywe maji.

“Mmetueleza ipo changamoto ya mradi kukaa muda mrefu bila kukamilika na nyingine ni ya kibajeti ambapo mlitoa ombi kwamba kuna kiasi cha milioni 400 hazijafika,tunatamani tupate ile barua ambayo mliielekeza kwa Wizara,kupitia Mwenge wa Uhuru, tuweze kumkumbusha Waziri, ili kama fedha hiyo imeshapatikana ije mara moja kwa ajili ya utekelezaji wa mradi na wananchi wapate maji,”ameeleza Mnzava na kuongeza kuwa

“Tunaomba hiyo barua leo, tumjulishe Waziri leo ili atupe majawabu.na atueleze mipango imekaaje wizarani ili kupata fedha hizo ili wananchi wapate maji,”.

Akisoma taarifa Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza, amesema lengo la mradi huo ni kutoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Kata ya Kwediyamba wapatao 5,746 na unatekelezwa na HTM kwa kutumia wataalam wa ndani (Force
Account).

“Mradi ulianza kutekelezwa Septemba 11, 2022 na ulitegemewa kukamilka Septemba 10, 2023,kutokana na fedha kutopatikana kwa wakati haujakamilika hadi sasa na utagharimu kiasi cha zaidi ya bilioni 1.2 fedha toka Serikali Kuu hadi sasa mamlaka imepokea milioni 800 kwa awamu tatu kuanzia mwaka wa fedha 2022/23 na 2023/24 huku unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2024,”.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza (wa pili kulia) wakati akionesha michoro ya mradi wa maji Kwediyamba

Ameeleza kuwa kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na ufungaji wa pampu ya kusukumia maji, kuchimba mtaro na kulaza bomba kuu la kipenyo cha milimita 110 (PN16 & PN10)
umbali wa mita 5,925, ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 kwenye mnara wa mita tisa katika mtaa wa Mpakani.

Pia kuchimba mtaro na kulaza mtandao wa mabomba ya kusambaza maji ya vipenyo kuanzia milimita 32 hadi 160 (PN 12.5 & PN10) kwa umbali wa mita 17,920, ujenzi wa vituo/vilula 29 vya kuchotea maji.

Mhandisi Mgaza amesema, wananchi wamechangia mradi kwa kutoa maeneo yao bure yenye ukubwa wa zaidi ya nusu hekari yenye thamani ya milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mradi.

Aidha amesema kuwa kiasi cha milioni 800 zimetumika zote kutekeleza shughuli za usanifu wa mradi na maandalizi ya michoro, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 150,000 kwenye mnara wa mita tisa, kuchimba mtaro na kulaza bomba kuu la kipenyo cha milimita 110 (PN16, PN 12.5 na PN10) umbali wa mita 5,925, kuchimba mtaro na kulaza bomba kuu la kusambazia maji (Distribution main) kipenyo cha milimita 150 (PN 12 na PN10) umbali wa mita 2,000.

Tenki la maji Kwediyamba

Pamoja na kuchimba mtaro na kulaza bomba la kusambaza maji lenye kipenyo cha milimita 63, milimita 50, na milimita 32 (PN10) umbali wa mita 1,650.

“Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 70. ili kukamilisha inahitajika milioni 478.6 kwa ajili ya ununuzi na ulazaji wa mabomba,ujenzi wa vituo na chemba pamoja na gharama za usimamizi,mamlaka umeandika barua kuikumbusha Wizara kiasia hicho cha fedha,”.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (wa nne kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa kwenye mradi wa maji Kwediyamba. Mwenge ulikimbizwa Mkoa wa Tanga kwa siku 11 Kushoto ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Handeni, Mhandisi Hosea Mwingizi
Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza akisoma taarifa ya Mradi wa Maji Kwediyamba