January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilimanjaro bado inakabiliwa na changamoto ya wanawake kumiliki ardhi

Na Martha Fatael, Moshi,timesmajira

SERIKALI imeutaja mkoa wa Kilimanjaro kuwa bado unakabiliwa na changamoto za kumnyima mwanamke fursa ya kumiliki ardhi kama ilivyo takwa la katiba ya nchi.

Ibara ya 24 ya katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na anayohaki ya kulindiwa mali yake kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza jana ,Mkuu wa wilaya ya Same, Edward Mpogolo amesema hayo akipokea msafara wa kitaifa wa kusherehekea siku ya mwanamke wa kijijini inayokwenda sanjari na Siku ya chakula Duniani inayofanyika kitaifa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ametaka jamii ya wakazi wa mkoa huo kubadili fikra na kumpa thamani mwanamke kwa kuhakikisha anapatiwa haki hiyo kama ilivyo kwa wanaume.

Mpogolo amesema kwa sasa serikali imeboresha huduma za afya, elimu, upatikanaji wa uhakika wa Umeme vijijni na barabara ili kupunguza tamaa ya watu kuhama vijijni na kukimbilia mjini.

Amesema zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanaishi vijiji na serikali imeelekeza nguvu kubwa katika kuboresha maisha ambayo yanamgusa mwanamke kwa asilimia kubwa.

Akizungumzia msafara huo ulioanzia jijini Mwanza, kutoka Tahea, Musa Masongo amesema katika msafara huo wameelimisha jamii kuhusu haki zao za kumiliki ardhi na kumthamini mwanamke wa kijijini.

Aidha msafara huo ulioandaliwa kwa kushirikiana na wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto, wamebaini kuwepo kwa ukatili wa kijinsia na kutaka mabadiliko ili kumsaidia mwanamke.