November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki mkoani Kilimanjaro mwaka 2005-2015 Anne Kilango (kulia), amechukua fomu leo Julai 15, 2020 ili kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kuteuliwa kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kushoto ni Katibu wa CCM Wilaya ya Same, Victoria Mahembe akimkabidhi Kilango fomu hiyo. (Picha na Yusuph Mussa).

Kilango achukua fomu kumkabili Kaboyoka wa CHADEMA

Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Same

ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya CCM Anne Kilango amejitosa kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni za chama hicho baada ya kuchukua fomu ya kuwania kupeperusha bendera ya CCM Jimbo la Same Mashariki.

Kilango ambaye ni Mbunge mwenye ushawishi mkubwa awapo bungeni, na hasa kwenye hoja zake, alichukua fomu hiyo leo katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Same, huku akikabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CCM Wilaya ya Same Victoria Mahembe.

Kilango ambaye amekuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi viwili mfululizo mwaka 2005 hadi 2015, kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, aling’olewa na mpinzani wake wa ‘jadi’ Naghenjwa Kaboyoka kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kaboyoka kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, katika kura za maoni aligombea akiwa ndani ya CCM, lakini alibadilisha ‘gia angani’ na kwenda upinzani chama cha CHADEMA, ambapo alimtingisha vilivyo Kilango, lakini mwisho wa siku, Kilango alishinda.

Ndipo mwaka 2015, huku CHADEMA ikiwa na nguvu mpya ya aliyekuwa mgombea urais kupitia CHADEMA kama sio UKAWA, Edward Lowassa, tena helkopta ya CHADEMA ikienda kufanya kampeni kwenye jimbo hilo, Kilango aling’oka na kumuachia Kaboyoka.