Na Joyce Kasiki, Tanga
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimebuni kifaa cha kiteknolojia kinachojulikana kwa jina la Maxwell Truck Ghala kinacholenga kuwasaidia wakulima kufuatilia na kudhibiti hali ya mazao baada ya kuvuna, hususan mabadiliko ya unyevunyevu na joto yanayoweza kusababisha uharibifu wa mazao yaliyohifadhiwa.
Kifaa hicho, kinakusanya taarifa muhimu kuhusu mazingira ya uhifadhi wa mazao na kumsaidia mkulima kubaini mapema viashiria vya unyevunyevu, joto, ukungu (mold) na wadudu kabla mazao hayajaharibika.
Akieleza kuhusu ubunifu huo katika maonyesho ya Elimu Ujuzi na Ubunifu 2026 katika viwanja vya shule ya awkondari Usagara jijini Tanga ,Mhadhiri Msaidizi kutoka UDOM Jospeter Kaizilege amesema changamoto kubwa inayowakabili wakulima baada ya kuvuna ni mabadiliko ya unyevunyevu wakati mazao yanapokuwa yamehifadhiwa kwa muda mrefu.
Amesema mabadiliko hayo yanaweza kusababisha mazao kupata ukungu na kuharibika, hali inayoweza kumwingiza mkulima katika hasara endapo alikuwa amepanga kuyauza baada ya miezi kadhaa.
“Baada ya kuvuna na kuweka mazao ghalani, changamoto kubwa ni mabadiliko ya unyevunyevu. Mazao yakikaa muda mrefu yanaweza kuanza kupata ukungu,” amesema.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mfumo huo unamwezesha mkulima kupata taarifa kuhusu hali ya mazao bila kutegemea ukaguzi wa kawaida pekee, ambao unaweza kuchukua muda na kushindwa kubaini mabadiliko ya mazingira kwa wakati.
Amesema kifaa hicho tayari kimeanza kutumika kwa baadhi ya wakulima na kimeonyesha matokeo mazuri, huku UDOM ikiendelea na jitihada za kukitangaza na kukifikisha kwa wakulima zaidi katika mikoa mbalimbali.
“Tumeanza kufanya kazi na mkulima mmoja na kifaa kinampa matokeo mazuri. Pia tumeanza kukitangaza hapa Tanga, huku kwa wale wa Dodoma tumeanza kufanya nao kazi kupitia NFRA,” amesema.
Ubunifu huo unalenga kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna kwa kuwapa wakulima taarifa za wakati kuhusu mazingira ya uhifadhi, hatua inayoweza kuwasaidia kuchukua hatua mapema kabla mazao hayajaharibika na kupoteza thamani ya soko.

More Stories
UDSM yatambuliwa kwa Machapisho Bora
VETA yatengeneza Simu yake ya kwanza
Serikali:Elimu ya ujuzi yaanza kuzaa matunda