May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kesi ya Msanii Idris, Mwenzake kuanza kusikilizwa Agosti tano

Na Grace Gurisha, Times Majira Online, Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatarajia kuanza kusikiliza kesi ya kushindwa kusajili laini ya simu iliyokuwa inamilikiwa na mtu mwingine inayowakabili msanii wa vichekesho, Idriss Sultan (27) na Innocent Maiga, Agosti 5, mwaka huu.

Jumla ya mashahidi 15, wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo, ambapo leo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).

Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu wa mahakamani hiyo na kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya PH, ambapo aliwasomea upya washtakiwa hao mashtaka yanayomkabili.

Mitanto amedai kati ya Desemba 1, 2019 na Mei 19, 2020 katika eneo la Mbezi beach, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Idriss alitenda kosa la kushindwa kufanya usajili wa laini ya simu inayotumiwa na mtu mwingine.

imedaiwa katika kosa hilo mshtakiwa alitumia kadi ya simu iliyomilikiwa na Innocent Maiga bila kuripoti kwa mtoa leseni.

Katika shtaka la pili, Maiga anadaiwa kutenda kosa la kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya kadi ya simu kutoka kwake kwenda kwa Idriss kosa analodaiwa kulitenda kati ya Desemba 1, 2019 na Mei 19, mwaka huu eneo la Mbezi Beach Kinondoni jijini Dar es Salaam.

” Mei 5, mwaka huu Mkuu wa Upelelezi Kinondoni alipewa taarifa kwamba Idriss anatumia kadi ya simu ya Vodacom ambayo haijasajiliwa kwa jina lake na kwamba alitakiwa kuripoti Kituo cha Polisi Oysterbay na alifanya hivyo.

Inadaiwa polisi walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwa Idriss na kubaini uwepo wa laini hiyo ya simu na kwamba alikuwa akiitumia kwa mawasiliano yake ya kila siku licha ya kusajiliwa kwa jina la Maiga.

Ilidaiwa Idriss alikiri kutumia kadi hiyo ya simu ambayo ilikuwa ikimilikiwa kabla na Maiga na kwamba alikiri kuitumia tangu Desemba mwaka jana.

Maiga alidaiwa kukiri kumiliki kadi hiyo na alimpatia Idriss aweze kuitumia na kwamba alikiri kutoripoti kwenye mamlaka kuhusu mabadiliko ya kadi hiyo.

Hata hivyo, washitakiwa hao ambao wanawakilishwa na Wakili Jebra Kambole na Maria Mushi, walikiri maelezo yao binafsi pamoja na mashitaka yanayowakabili mahakamani hapo na kukana maelezo ya mashitaka.

Upande wa mashitaka ulidai wataleta mashahidi 15 na kama watahitaji kuongeza au kupunguza mashahidi wataieleza mahakama na kwamba wataeleza idadi ya vielelezo watakavyokuwa navyo kesi itakapoendelea.