April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT

Na Israel Mwaisaka, Rukwa

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Nkasi kimetaja changamoto mbali mbali za walimu, kama vile kutopandishwa madaraja, kutolipwa madai yao kwa wakati, na kutokuongezewa mishahara, kuwa sababu kuu za msongo wa mawazo miongoni mwa walimu nakupelekea kusababisha ukosefu wa ufanisi kazini.

Hayo yameelezwa na Mwalimu Daniel Mpepo Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania Wilaya ya Nkasi(CWT) kwenye ziara ya kutembelea shule za sekondari na kusikiliza kero pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili walimu ambapo ziara hiyo inaratibiwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kushirikiana na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi.

Mpepo amesema kuwa, kutosikilizwa kwa walimu changamoto zao kwa muda mrefu, limekuwa tatizo kubwa linalochangia msongo wa mawazo, walimu wanahitaji kuhakikishiwa kuwa madai yao, haki zao za ajira, na masuala mengine muhimu yanashughulikiwa kwa wakati ili kuboresha hali yao ya kazi na maisha.

Kwa upande wake mwalimu Mustafa Mitago ambae ni katibu wa Chama cha walimu Tanzania Wilaya ya Nkasi (CWT) ambaye amesema kliniki hii imetajwa kama suluhu ya kutatua changamoto za walimu na matarajio ni kuona walimu wanafikiwa na huduma hii ambapo amekiri kuwa kutosikilizwa kwa walimu kwenye changamoto zao imetajwa kuwa moja ya tatizo, kwani walimu wanakabiliwa na msongo wa mawazo huku akitoa wito kwa walimu kujitokeza kwa wingi kushiriki kliniki hii na kueleza changamoto zao ili kusaidia kuboresha mazingira ya kazi na kupunguza mzigo wa kiakili unaotokana na matatizo yanayowakabili.


Nao baadhi ya walimu waliowasilisha kero zao akiwemo mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mkole Allyshaka Husein amesema Kliniki hiyo Maalum ya kusikiliza kero za walimu itakuwa suluhisho la kusaidia kutatua changamoto na kero mbalimbali za walimu shuleni kwa kusogeza huduma karibu na maeneo yao, kwani walimu wamekuwa na msongo wa mawazo kutokana na kero mbalimbali ikiwemo kutopandishwa madaraja,pamoja na kutoongezewa mishahara na kutolipwa madai yao kwa wakati.