April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.

Na Moses Ng’wat, Mbozi

MKUU wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amewataka viongozi wa mitaa na kata kuongeza umakini katika kuhakikisha usalama wa maeneo yao kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika mara wanapobaini uwepo wa wageni wasiowafahamu au watu wanaowatilia mashaka.

Mbega alitoa wito huo Aprili 22, 2026, wakati wa kikao cha Baraza la Mamlaka ya Mji Vwawa kinachofanyika kila baada ya robo mwaka kwa lengo la kujadili maendeleo na changamoto zinazohusu ustawi wa wananchi.

Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi wa maeneo yao ni nguzo muhimu katika kudumisha amani na usalama, akibainisha kuwa kila mmoja ana wajibu wa kushiriki kulinda eneo analoishi.

Aidha, Mbega alisema katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo ongezeko la watu kutoka nchi jirani wanaoingia Wilaya ya Mbozi na kujihusisha na shughuli mbalimbali bila kufuata taratibu maalum, hali ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa taifa iwapo haitadhibitiwa mapema.

Aliongeza kuwa ni muhimu kwa viongozi wa mitaa kuwa makini na kuhakikisha wageni wote wanaingia na kuishi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na serikali, ili kuzuia matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wa wananchi.

Mwisho.