November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kanisa lafungiwa kuendesha ibada tata

Na Judith Ferdinand, Timesmajira online,Mwanza

Serikali wilayani Misungwi mkoani Mwanza imelifungia Kanisa la Lulembo lililopo katika Kijiji cha Nyamayinza ambalo licha ya kuendesha shughuli zake kinyume cha sheria kwa kutumia kibali cha tiba asilia pia linadaiwa kuzuia waumini wake kupata matibabu kwenye hospitali.

Huku ikibainika kuwepo kwa wodi bubu za wagonjwa kwenye nyumba za udongo zinazozunguka kanisa hilo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Paulo Chacha kubaini uwepo wa kanisa ili linaloendesha ibada tata.

Mkuu huyo wa Wilaya amebaini uwepo wa kabisa hilo Juni 8, mwaka huu katika kijiji cha Nyamayinza Kata ya Gulumungu wilayani humo huku akiliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili kubaini kama kuna watu waliofariki na kuzikwa katika eneo hilo kinyemela.

Amesema kanisa hilo linamilikiwa na William Masuma na mkewe, Kabula Lushika linaloendeshwa kwa kibali cha huduma ya tiba asili ambalo wamebaini kuendesha shughuli za maombezi kwa zaidi ya miaka mitano kwa kupokea mamia ya wagonjwa na kuwataka kuishi kwa maombi katika eneo hilo huku wakizuiliwa kwenda hospitalini kwa madai kuwa watapona kwa miujiza.

Amesisitiza kuwa kanisa hilo lisitumike tena kwa sababu hawana kibali cha kuendesha kanisa huku akiliagiza Jeshi la Polisi wafanye utafiti kubaini kama kuna makaburi hapo au hayapo kwani inawezekana kuna ndugu wanazikwa na watu hawana habari.

Amesema kuwa kuna mama alizaa watoto pacha kwenye Kituo cha Afya akaletwa huku hali ikabadilika badala arudishwe hospitalini akaletwa kulaza hapo akafa ambapo mama huyo ameacha watoto wadogo.

“Watu wanakufa hapa ninyi hamna taarifa wala hamjui, tumeshuhudia wagonjwa walivyo wengi eneo hili, hivi hawa mkiwaangalia kwa hali zao wanahitaji maombi au kupelekwa hospitalini kupatiwa matibabu,”.

Sanjari na hayo Chacha ameagiza wagonjwa wote walikutwa taabani kupelekwa katika kituo cha afya Misasi kwa ajili ya matibabu na uangalizi.

Mmoja wa wagonjwa waliokuwa katika eneo hilo Petro Lunalika,amesema alifika hapo Januari akisumbuliwa na tatizo la moyo.

“Nilienda hospitalini wakaniambia nina tatizo, nmekuja hapa na kufanyiwa maombi sasa hivi nimepona,” amesema Lunalika

Naye Juma Emmanuel, amesema kuwa walisikia taarifa kuwa pale kuna maombi na mtu yoyote anayeugua analetwa hapo, hivyo akampeleka mjomba wake katika neneo hilo miezi mitatu akiwa haoni, sasa anaendelea vizuri wala hajawahi kusikia mtu yoyote amefariki.

Ameongeza kuwa wagonjwa wanaofika kutibiwa katika eneo hilo hupatiwa eneo kwa ajili ya kujenga makazi yao bila kujali yatakuwa na ubora wala usalama wao.

Akizungumza akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, William Masuma amesema pamoja na kuwa na kibali cha kutoa huduma ya tiba asili, katika eneo hilo anatoa huduma ya maombezi kwa wagonjwa pekee.

“Mimi hapa sitibu wagonjwa ila ninawaombea tu wanapona,sina huduma nyingine ya ziada ninayoitoa hapa zaidi ya maombi,” amesema Masuma.