June 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yaridhishwa utekelezaji miradi 

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza 

KAMATI  ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),imesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta mbalimbali umeendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Akizungumza Juni 20,2026 wakati wa ziara ya kamati hiyo kukagua miradi inayotekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Florent Kyombo,alipongeza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo ambapo  alisema imekuwa na mchango katika kuboresha huduma na maisha ya wananchi.

Amesema kamati imeridhishwa na maendeleo ya miundombinu ya barabara na miradi mingine ya huduma za jamii inayotekelezwa katika halmashauri hiyo, huku akiitaka  kuendelea kushughulikia maeneo machache yanayohitaji maboresho.

Hata hivyo,amewataka wakandarasi wanaotekeleza baadhi ya miradi kuongeza kasi ya kazi ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati uliopangwa.

Sanjari na hayo amesema mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Ibungilo, unaotekelezwa na kampuni ya SUMA JKT, utasaidia kuboresha huduma za afya katika halmshauri  hiyo.

Hata hivyo  Kyombo,ameipongeza halmshauri hiyo kwa jitihada za kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi yake katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya elimu huku akitolea mfano mradi wa ujenzi wa  shule ya sekondari Kahasa kuwa umedhihirisha matumizi mazuri ya mapato ya ndani.

Huku  ameitaka halmashauri hiyo  kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule hiyo ili kuongeza usalama wa wanafunzi na mali za shule.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu, amesema atafanyia kazi mapendekezo mbalimbali yaliotolewa na Kamati hiyo kwa ajili ya kukamilisha miradi kwa wakati na kuhakikisha inawaletea maendeleo wananchi.