Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23 ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Najma Giga Machi 23, 2022 katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe kujadili na kuridhia bajeti katika kikao kilichohusisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Wakurugenzi wa Idara mbalimbali, wataalamu na taaisisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Tunashukuru kwa wasilisho la Bajeti hii na wajumbe wamesikiliza wamepata nafasi ya kutoa maoni yao katika maeneo mbalimbali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu na shughuli za serikali kufanyika bila kikwazo na wajumbe wote wa kamati wameipitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu,”alisema Najma.
Awali katika kikao hicho Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana aliwasilisha taarifa kuhusu Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23 mbele ya kamati hiyo.
Pia Pindi alieleza mpango wa shughuli zitakazotekelezwa kwa kutumia bajeti hiyo ya mwaka wa fedha ujao 2022/23 ambapo wanakamati kwa kauli moja walipitisha randama ya bajeti na kutoa ushauri kwa wizara katika baadhi ya maeneo yanayohitaji kufanyiwa marekebisho.
“Nitumie nafasi hii kuishukuru kamati na wajumbe kwa mawazo yao hadi kupitisha bajeti hii na nimshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu bajeti hii tunayopitisha hapa lazima ipate ridhaa ya Mkuu wetu wa Nchi,”
Aidha alibainisha kuwa kupitishwa kwa bajeti hii kunatoa fursa ya utekelezwaji wa malengo, dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2020/25, utekelezaji wa Ilani na hatimaye kupitia Bunge kila mwananchi apate maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa.
Akitoa elimu ya uelewa kuhusu muundo na utekelezaji wa majukumu Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Katibu Mtendaji Dkt. Godwill Wanga alibanisha kwamba kupitia baraza hilo wapo katika mchakato wakuunganisha mifumo ya Taasisi zote zinazohudumia wafanyabiashara na kuwa mfumo mmoja utakaosaidia wafanyabishara kufanya shuhuli zao kwa urahisi na kutatua changamoto zinazowakabili.
“Utafiti ulifanyika namna ya kuunganisha mfumo kwa sababu iliyopo inaonyesha kuleta changamoto kwa wafanyabiashara maana kwa sasa kila taaisisi ina mfumo wake hivyo maelekezo yaliyotolewa ni kuiunganisha pamoja na taarifa zake ambapo mtu wa NIDA au BRELA akitaka anaingia kwenye data base hiyo hiyo na kupata taarifa anazozitaka ambapo hatua hii itaondoa usumbufu kwa wafanyabiashara,” alieleza Dkt. Wanga.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini