November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yamfuta machozi mnufaika wa TASAF

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wametembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Wilayani Uyui Mkoani Tabora na kuguswa na mmoja wa wanufaika kwa jinsi alivyopiga hatua kubwa.

Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe wenzake baada ya kutembelea miradi ya bwawa na kisima cha maji ya kunywa katika Kijiji cha Magiri, Kata ya Magiri, Wilayani humo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Florent Kyombo alieleza kufurahishwa na miradi hiyo lakini akaguswa kipekee na Bibi Amina Idd (73).

Bibi huyo ambaye ni mjane ameweza kuanzisha miradi midogo 2 (wa kuuza kahawa na kibanda cha biashara) kupitia fedha kidogo anayopata kutoka TASAF, miradi hiyo imemsaidia kuanza kujenga nyumba ya kuishi ya tofali za kuchoma.

Makamu Mwenyekiti alimpongeza kwa kutumia vizuri fedha kidogo anayopata hadi kufikia hatua ya kuanza kujenga kidogo kidogo nyumba ya makazi yake.

‘Bibi tunakupongeza sana kwa kufikia hatua hii nzuri, hakika umeonesha mfano mzuri wa jinsi mpango huu wa serikali unavyoweza kusaidia jamii kujikwamua kiuchumi, na sisi tutakuunga mkono ili umalize nyumba yako haraka’, alisema

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Wajumbe wa Kamati hiyo na msafara wao pamoja na wataalamu wa halmashauri na viongozi wa Chama tawala Wilayani humo walimchangia papo hapo jumla ya sh 532, 000 ili kumalizia nyumba yake.

Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt John Mboya aliieleza Kamati kuwa siku chache zilizopita walimtembelea bibi huyo na kuguswa pia na juhudi zake ambapo yeye binafsi aliahidi kumnunulia bati zote zilizobaki huku Mkurugenzi Mtendaji wa hamashauri hiyo Hemed Magaro akiahidi kumalizia kuweka madirisha na milango.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Jenista Mhagama alisema hadi sasa zaidi ya sh bil 12 zimeshaletwa katika wilaya hiyo kupitia mpango huo na zaidi ya bil 9 zimeshagawiwa kwa walengwa.

Aliongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha kaya maskini zote zinatambuliwa na kuingizwa katika mpango huo na hata zile ambazo ziliondolewa kimakosa zitahakikiwa upya, zitakazokidhivigezo zitarejshwa..

Mwenyekiti wa CCM Wilayani hapa Lubasha Makoba alipongeza Kamati hiyo kwa kazi nzuri wanayofanya na kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mpango huo ili kuinua maisha ya wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Florent Kyombo (wa tano kutoka kulia) akiwa na Wajumbe wenzake wa Kamati ya Kdumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria jana na Viongozi wa chama na serikali, wakiwa nyumbani kwa mnufaika wa TASAF Bibi Amina Idd (73) Wilayani Uyui Mkoani Tabora jana. Picha na Allan Vicent