May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaim:Haipendezi wenyeji kunyimwa miradi ya maendeleo

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Ileje.

WATENDAJI wa serikali nchini ambao wamepewa dhamana ya kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo wametakiwa kuhakikisha kuwa wanatoa kipaumbele cha ajira na zabuni kwa watu wanatoka kwenye eneo kunakotekelezwa mradi husika badala ya fursa hiyo kuwapa watu wa nje ya mradi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Wilaya ya Ileje lililojengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 237.36 mjini Itumba Wilayani hapa, kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Abdalla Shaibu Kaim amesema haipendezi kuona watendaji wa serikali waliopewa dhamana ya kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo wanatoa fursa ndogo ndogo kama kukusanya mchana na kokoto kwa wageni wanaotoka nje ya mradi badala ya kuwapa wenyeji.

“Niombe kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo zile fursa ndogo kama kukusanya mchana na kokoto wapewe wenyeji washirikishwe ili nao waweze kunufaika kwani haipendezi kuona fursa hizo wanapewa watu kutoka nje ya mradi” amesisitiza Kaim.

Pia kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 2023, ametaka kazi zote zisizo za kitaalam wapewe vijana na wakazi wa maeneo kunakofanyika mradi ili nao waweze kunufaika na fursa hizo za miradi kufanyika katika maeneo yao.

Akizungumzia kuhusu Hospitali hiyo baada ya kufanya ukaguzi na kuzindua jengo hilo la wagonjwa mahututi , Kiongozi huyo wa mbio za mwenge licha ya kuzindua na kuridhia jengo hilo kuanza kutoa huduma, alitoa siku tatu kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya kufanya marekebisho kasoro zilizobainika katika ukaguzi wa jengo hilo.

Aidha, Kaim amewata watumishi hao wa sekta ya afya kutekeleza majukumu yao kwa upendo bila kusahau maadili na miiko na ili wanachi wafaidike.

Ukiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mwenge wa uhuru umepitia miradi nane yenye thamani kya shilingi za kitanzania bilioni 2.027 ambapo yote imekubaliwa na Mwenge huo kuendelea na utekelezaji wake.

Mwenge wa Uhuru leo Septemba 6, 2023 umekamilisha mbio zake Mkoani Songwe kwa kukimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje na siku ya Septemba 7, 2023 utakabidhiwa Mkoani Mbeya.