November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JPM : Tupeni tena miaka 5 tufanye makubwa zaidi

Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Dkt.John Magufuli amesema uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu ni muhimu kwa Taifa hivyo ni vyema kuchagua CCM ili kumalizia awamu ya pili ya utekelezaji wa ilani yao.

Pia ameomba kura kwa vyama vyote nchini wakiwemo watanzania ambao hawana vyama kumpa kura ya ndiyo ili kukamilisha muhula wake wa pili wa utekelezaji wa miradi mikubwa aliyoanzisha.

Akizungumza leo katika uzinduzi wa kampeni na Ilani ya chama hicho 2020/25,Dkt,Magufuli amesema,chama pekee cha kuleta amani na mapinduzi ya kimaendeleo ni CCM.

Dkt,Magufuli ambaye pia ni Rais anayemaliza muda wake amesema,maendeleo ya nchi hayana chama hivyo amejitoa kwa ajili ya Taifa na kuomba kura za ndiyo kwa watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.

“Uchaguzi huu ni muhimu sana kwetu ambao unapelekea kuamua kupata viongozi wa dhati ambao watakwenda kuwatumikia watanzania na siyo viongozi wenye ajenda zao binafsi na kubeba maslahi ya watu wengine ,”amesema na kuongeza kuwa

“Uamuzi ni wenu naomba mtakafari kwa maslahi mapana ya Taifa kwani uchaguzi huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya watanzania na nchi kwa ujumla.”

Akizugumzia miongoni mwa mambo yaliyopangwa kutekelezwa katika ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 amesema ni pamoja na kusimamia misingi ya kisera ,kisheria na kanuni za usimamizi wa sekta ya fedha .

Amesema katika miaka mitano serikali ya CCM itaendelea kuweka msisitizo katika kujenga sekta binafsi iliyo bora inayoshirikiana na serikali katika kutoa mchango wenye manufaa kwa Taifa pamoja na kuisimamia serikali ili kuhakikisha watendaji wanakuwa na mtazamo chanya juu ya sekta binafsi.

Aidha amesema katika kipindi hicho CCM kitaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha wananchi kuwekewa mazingira mazuri ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo .

Pia katika kipindi hicho amesema CCM kitaelekeza serikali kuongeza fursa za ajira katika sekta isiyo rasmi .

Amesema pia kitasimamia kilimo kuhakikisha kinakuwa chenye tija kitakachowafanya watu wafanye biashara  na kujipatia masoko pamoja na kuongeza kipato chao.

Katika ilani yao pia imesema,wanatarajia kuongeza ndege tano miongoni mwa ndege hizo,moja itakuwa kwa ajili ya kubeba mizigo.

“Nitahakikisha kitu cha kwanza cha kuanza nacho hapa makao makuu ya nchi ni kujenga uwanja mkubwa  kwa ajili ya shughuli za matukio mbalimbali,”amesema