Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
JOTO la watia nia wanaotaka kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania ubunge majimbo ya Lushoto, Mlalo na Korogwe Vijijini limezidi kupanda baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Riziki Shemdoe kuchukua fomu.
Profesa Shemdoe amechukua fomu hiyo Juni 30, 2025 kwenye Ofisi ya CCM Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kwa ajili ya kuwania ubunge Jimbo la Lushoto ili kumvaa Mbunge wa sasa Shaaban Shekilindi.
Profesa Shemdoe ambaye hadi anatangaza nia alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu TAMISEMI, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

Mwingine anaetaka Jimbo la Lushoto ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Mathew Mbaruku. Pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, pia alikuwa Diwani wa Kata ya Magamba, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo Lushoto, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi WIlaya ya Lushoto, na Mwenyekiti wa Kijiji cha Magamba kwa miaka 20.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa Amiri Mkufya maarufu kama AMESCO, ni miongoni mwa watia nia Jimbo la Mlalo, ambaye naye amechukua fomu kwa ajili ya kumkabili Mbunge wa sasa Rashid Shangazi.

Pamoja na kuwa kada, Mkufya pia ni mshindi wa tuzo za Young CEO Round table Africa, Mchumi na msomi kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kutoka Jimbo la Korogwe Vijijini, Mwajuma Mohamed ambaye hivi karibuni amechaguliwa kwa kishindo kuwa Mjumbe wa Bodi wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), amechukua fomu ili kumvaa Mbunge wa sasa wa jimbo hilo Timotheo Mnzava.
Mohamed ambaye ni mwanaCCM kindakindaki, pia ni Kiongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Tanga, amekabidhiwa fomu ya kuwania kuteuliwa ili kugombea ubunge Jimbo la Korogwe Vijijini Juni 30, 2025.




More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako