November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKT yatoa wito kwa vijana waliomaliza kidato cha sita kuhudhuria mafunzo ya Jeshi

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

JESHI la kujenga  Taifa ( JKT ) limetoa wito kwa vijana waliohitimu elimu ya Sekondari Kidato cha sita kwa mwaka 2022 kutoka shule za Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya jeshi hilo kwa mujibu wa Sheria.

Vijana hao wamepangiwa kuripoti makambini kuanzia June 3 hadi 17 mwaka huu katika kambi mbalimbali ikiwemo  kambi ya JKT Rwamkoma mkoani Mara,JKT Msange Tabora,JKT Ruvu Pwani,JKT Mpwapwa na Makutupora JKT Dodoma. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,Mkuu wa Tawi la Utalawa  kutoka Jeshi la Kujenga Taifa Brigedia Jenerali, Hassan Mabena amesema kambi nyingine vijana hao watakayo kwenda ni JKT Mafinga Iringa,JKT  Mlale Ruvuma,JKT Mgambo,JKT Maramba  mkoni Tanga,JKT Makuyuni Arusha, JKT Bulombora,JKT Kanembwa,JKT Mtabika mkoani Kigoma.

Ametaja kambi nyingine ni  JKT Itaka Songwe,JKT Luwa,JKT  Milundikwa Rukwa,JKT Nachingwea Lindi ,JKT Kibiti Pwani pamoja na Oljoro JKT Arusha.”Wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho wanapaswa kutipoti katika kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandiszi Mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo,”amesema Brigedia Jenerali Mabena

Amesema jeshi hilo linawataka vijana hao kuripoti  wakiwa na vifaa mbalimbali huku orodha kamili ya majina ya vijana hao walioitwa makambi ya JKT  yapo katika   tovuti ya jeshi hilo.

Brigedia Jenerali Mabena amesema Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele aliwakaribisha vijana walioitwa ili waweze kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo,Umoja wa kitaifa ,Stadi za kazi ,Stadi za Maisha na Utayari wa kulijenga na kulitumikia taifa.