Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Pwani
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limeanza ufugaji wa samaki katika kikosi
cha Ruvu JKT ambapo mpaka sasa lina vizimba 25 vyenye samaki zaidi ya
87,000 huku lengo la ufugaji huo ni kwa ajili ya kulisha vijana na askari wa Jeshi hilo pamoja na kuwauzia wananchi.
Akizungumza na wandishi wa habari alipotembelea kikosi hicho na kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo ufugaji wa samaki wa kutumia vizimba unaofanywa na kikosi hicho kilichopo Ruvu mkoani Pwani,Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema ,jeshi hilo lina mpango wa kuongeza zaidi vizimba vya samaki ili kuongeza tija zaidi katika uzalishaji wa samaki.
“Ili kufikia malengo hayo ,tunahakikisha samaki hawa tunawafuga kwa kutumia teknolojia ya kisasa pamoja na kuwapa chakula bora ambacho kitawawezesha kukua vizuri na kuzaliana kwa wingi.”amesema Brigedia Jenerali Mabena
Hata hivyo amesema,changamoto inayowakabili hivi sasa ni uhaba wa mvua
ambapo walitarajia zitakuwa nyingi lakini imekuwa tofauti hali iliyosababisha kuwavuna samaki hao kabla ya muda wa miezi sita ambao ndio walitarajia kuanza kuwavuna.
“Tumelazimika kuvuna samaki kabla ya muda ili kupunguza idadi kwa
ajili ya kuwapa nafasi waliobaki waweze kuzaliana na kuwa na afya
bora,”amesema Brigedia Jenerali Mabena
Hata hivyo alisema wameweza kukabiliana na changamoto hiyo pale mvua
zitakapoanza kunyesha watahakikisha maji hayapotei kwa kujenga kingo za kuzuia maji yasipotee .
Kwa upande wake Mtaalam wa samaki katika kikosi hicho Sajenti Maulid Heri
amesema,mradi huo ulianza Machi 21 ambapo kuna vizimba 25 ambapo kila
kizimba kina samaki 3,500.
Amesema ,lengo lao ni kuwa na vizimba zaidi ya 100 ili
wawe na samaki wengi zaidi kwa ajili ya kuendelea kulisha vijana na askarui lakini pia kuwauzia wananchi wengine.
Aidha Sajenti Maulid amesema, mradi huo umegharimu sh million 134 na unatarajia kuingiza sh
milioni 200 mara baada ya kuanza kuwavuna .
Sajenti Maulid amesema samaki hao wanafugwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa itakayowawezesha kuwa na samaki bora na wenye kuzaliana vizuri na hatimaye kufikia matarajio yaliyokusudiwa na JKT.
“Na kwa kutumia teknolojia hiyo tumeanza kuzalisha vifaranga vya samaki kwa ajili ya
mbegu ambayo pia tutauza kwa wananchi wengine.”amesema
More Stories
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake