April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mil.7 zahitajika kwa ajilli ya watoto 22 wenye ulemavu

Na Esther Macha, Timesmajira,Online,Mbeya

ZAIDI ya shilingi milioni .7 zahitajika kwa ajili ya matibabu ya watoto 22 wenye ulemavu mbalimbali wakiwemo wenye usonji baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na madaktari wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Mwenyekiti wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Foundation Julitha Lukamata amesema kuwa watoto hao ni kutoka Kata ya Iyela pekee mkoani hapa.

“watoto hawa ni kata hii pekee tu na tuliwapata baada ya kupita nyumba kwa nyumba na kutoa elimu kwa wazazi na walezi ndo tukafanikiwa kupata idadi hiyo ya watoto wenye ulemavu  na wenye usonji “amesema.

Kwa upande wake Katibu wa Taasisi hiyo ,Stella Kita amesema watoto wengi wenye ulemavu wamekuwa wakifungiwa ndani kutokana na wazazi kushindwa gharama za mazoezi au matibabu hivyo kuona njia sahihi ni kuwafungia ndani pekee na wengine kunyimwa haki ya kupata elimu kutokana na kufungiwa ndani.

Akizungumzia matatizo hayo ya watoto ,Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Dkt .Godlove Mbwanji amesema walipokea ombi kutoka taasisi ya Funguka ili waweze kusaidiwa vipimo kwa watoto hao ambao wengi wao wanaishi mazingira magumu hivyo kama Hospitali wametoa mchango wa vipimo bure.

“Kutokana na mazingira magumu ya watoto hawa na wazazi kama hospitali tuliona hili jambo ni muhimu hivyo tukaamua kutoa vipimo bure kwa kuni hili la watoto wenye ulemavu wakiwemo wenye usonji amesema Dkt. Mbwanji

Lengo la Taasisi ya Funguka ni kuwafikia watoto wenye ulemavu katika Kata zote za Jijini Mbeya.

Baadhi ya wazazi akiwemo Julitha Lukamata amesema wazazi wengi wamekuwa wakikata tamaa ya gharama za vipimo na matibabu hivyo kuamua kuwafungia ndani lakini yeye hakukata tamaa na kuamua kumpeleka hospitali kwa kutumia bima ya afya.

Aidha Rose Sanga ameishukuru taasisi hiyo mara baada ya mtoto wake kupatiwa vipimo ndipo alipopata msaada kupitia Ustawi wa Jamii Jiji ambapo anapatiwa matibabu bure.