April 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jinsi Presha inayoathiri nguvu za kiume/Saikolojia

Na Aveline Kitomary,TimesMajira Online,Dar es Salaam.

UGONJWA  wa shikizo la juu la damu (presha ya kupanda) hutokea wakati nguvu ya msukumo  wa damu  katika mishipa ya moyo   huwa kubwa  kuliko kawaida .

Ongezeko hilo  husababisha moyo kufanya kazi  kupita kiasi ili kusukuma damu  katika mishipa ya damu .

Kwa kawaida ugonjwa wa presha hauna dalili  ili ukidumu kwa muda mrefu  bila ya tiba kuna madhara makubwa  kiafya .

Asilimia 95 ya wagonjwa wa presha ya kupanda hawana sababu zinazojulikana kisayansi .

Mara nyingi sababu zinazoainishwa ni historia ya ugonjwa katika familia ,uzito mkubwa ,matumizi ya chumvi nyingi,kutokufanya mazoezi ,uvutaji sigara ,ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi  na umri mkubwa.

Asilimia ya watu wanaopata ugonjwa presha  ya kupanda  huwa wanakuwa  katika kundi la magonjwa mbalimbali kama  figo,mishipa ya moyo  na mfumo wa homoni.

HALI ILIVYO

Katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tangu ilipoanzishwa Septemba 2015  hadi Aprili  2020  kati ya wagonjwa 334,774 waliotibiwa asilimia 66 ya wagonjwa walikuwa na tatizo la presha ya kupanda.

Ripoti ya JKCI inasema tatizo la linaongezeka kulingana na mabadiliko ya maisha ya watu ikiwa ni pamoja na mfumo wa ulaji na kazi.

Daktari Bingwa wa Moyo, Samwel Rweyemamu anasema katika tathimini kwa  maeneo ya mjini na vijijini  kunaongezeko la asilimia 30 na 35.

“ Lakini inategenmea na mahali mfano nilifanya  utafiti Songea nilivyofanya tathimini  wale watu waliopima takribani 800 asilimia 64 walikuwa na shikizo la damu.

“Lakini pia  hata Dar es Salaam shinikizo la damu linakaribia  kwenye asilimia 40 mfano JKCI tangu tumeanza ukiangalia asilimia 70 ni wagonjwa wanakuja wakiwa na shinikizo la  damu tatizo ni kubwa linaongezeka kila mwaka,”anabainisha Dk Rweyemamu.

AINA ZA PRESHA

Dk Rweyemamu anasema wakipima shikizo la juu la damu huwa wanaangalia rekodi mbili ambazo ni  systolic  na diastolic.

“Sistolic ikiwa iko sawa sawa na 140 au zaidi ni hatari  na diastolic  ikiwa 90 au zaidi tunasema  huyu mgonjwa anatatizo la  shinikizo la damu.

“ Shinikizo la damu  limegawanyika katika sehemu mbili kuna inayoitwa primary  high pertation au visababishi halisi  havijajulika lakini tunaangalia viashiria.

“Lakini aina ya pili tunaiita secondary high pertation ambayo inaweza kusababishwa na magonjwa  mengine  hapa mtu anapata presha kwasababu kuna magonjwa mengine ndani yake.

VISABABISHI

Anasema viashiria vya hatari  moja wapo uvutaji sigara,unywaji pombe kupindukia ,chakula hatarishi mfano kula chakula chenye chumvi nyingi au kuongeza chumvi kwenye chakula ,mafuta mengi.

“Inaweza kusababishwa na ulaji wa vitu vingi ambavyo ni hatari kwa afya mfano kuna vinywaji vyenye sukari nyingi  kama  soda, watu wanakula sana lambalamba kila gari ikipita watu wanalamba lamba vitu vyenye sukari mwisho siku itakuongezea uzito ulipindukia kwahiyo  kutumia sukari ni mmoja wapo.

“Lakini pia kushindwa kufanya mazoezi (sedentary life) wataalamu  wanapendekeza angalau kufanya mazoezi mara tatu kwa wiki ,kwa nusu saa unaweza kukimbia au kutembea,”anasema.

Anasema sababu nyingine ni ugonjwa wa figo kwani mtu akiwa na shida ya figo presha yake hupanda  na akiwa na shinikizo la damu pia anaweza kupata ugonjwa wa figo.

“ lakini wengine wanaweza kuwa na kansa ya tumboni mfano adrenal gland kansa inasababisha na pia tezi la kwenye shingo  ikiwa inatoa vichocheo kwa wingi  inakusababisha presha,”anabainisha.

HUATHIRI NGUVU ZA KIUME

Dk Rweyemamu anasema tatizo la shinikizo la juu la damu linaweza kuathiri nguvu za kiume.

“kwa wanaume zaidi sahivi kuna tataizo la nguvu  za kiume unakuta wengi wanakuja wanakuambia huko nyumbani familia  inalalamika kwasababu ya shinikizo la damu lakini pia kwasababu  ya madawa mengine yanasababisha ukosefu wa nguvu za kiume.

“ Hili ni shida inayojitokeza  ni jambo linaoneka  kama watu wanashindwa kulieleza vizuri lakini  watu walio wengi wanakuja,Hatujawahi kufanya  na utafiti  wa kuona tatizo hilo lipo kubwa kias gani lakini lipo,”anafafanua.

Anasema  Wanaume wanaougua shinikizo la juu la damu  wako hatarini kupungukiwa nguvu za kiume.

Dk Rweyemamu anaainisha madahara mengine kuwa ni moyo kuharibika ,kupata kiharusi ,figo zitaharibka,macho yataharibika.

WAGONJWA HUATHIRIKA SAIKOLOJI

Dk Rweyemamu anasema kuna uwezekanao wa wagonjwa kuweza kupata tatizo la kisaikolojia kulingana na mapokeo yao.

“Nilikuwa na  mgonjwa ambaye niliambiwa mwezi uliopita haongei  lakin  kwa sasa anasema kuwa anaona watu usiku mpaka leo hajalala kwenye familia. 

“hizo ni dalili za awali za kujua kuwa mgonjwa huyu sasa alikuwa  na presha  na mishipa ya moyo ikaziba na akafanyiwa oparationa hali  hiyo inamfanya anaanza kupata sonona (depression).

“ Sasa anaelekea kupata magonjwa ya akili kwahiyo tunaona alianaza na presha mishipa ya damu ikazaiba amefaniyiwa upasuaji sasa anaenda kupata sonona.

Anasema jinsi ya kuwasaidia watu wenye tatizo hilo ni kuwapeleka kwa mwanasaikolojia ili kupewa ushauri.

“Tunaangali jinsi ya kumsaidia kwa kumpeleka kwa msaikolojia anaweza kuta msaada, Tukiona mtu anaumuhimu wa kuhitaji saikolojia tunampeleka,”anaeleza.

UELEWA BADO MDOGO

Dk Rweyemamu anasema utafiti uliofanyka Simanjiro Mkoani Manyara na Kisiwa cha  Mafia kiasi cha uelewa ulikuwa  chini ya asilimia 50.

“ lakini tunatoa huduma ili watu wapate mwamko  lakini unakuta watu walio wengi wanashikizo la damu lakini hawaelewi kama wanashikio la damu.

NJIA YA KUEPUKA

Mfumo bora wa maisha unatajwa kuwa na nafasi kubwa zaidi katika kuepuka magonjwa  hasa magonjwa yasiyo ya  kuambukiza.

Dk Rweyemamu anataja  mfumo bora wa maisha kuwa suluhisho namba moja ya kuweza kuepuka na  presha na magonjwa moyo.

Anasema aina ya ulaji wa vyakula na jinsi ya ufanyaji mazoezi au kazi hufanya mwili kuwa katika hali ya kukabili magonjwa au kuepuka kabisa.

“Kuna aina ya vyakula na vinywaji mtu anatakiwa kuviepuka mfano kunywa  juisi kila wakati ,pipi na  vitu vingine vyenye sukari, kupunguza chumvi hivi ni muhimu sana kitabibu,na kingine mtu kupunguza uzito kama ni mkubwa kwasababu unaweza kutumia dawa za presha lakini kama wewe unakilo 150  hata nikikupa dawa za presha zikaisha zote  kurudi kawaida inakuwa ni vigimu sana.

 Anasema ni lazima kuweka uwiano mzuri wa afya ya mwili kutokana na dawa za presha siku zote ambazo mgonjwa ataishi

“Kwanza dawa  za presha au moyo hazikai mwilini au tumboni zikishatumika zinatoka kwa njia ya mkojo  kwahiyo mgonjwa anatakiwa kutumia dawa kila siku.

 “Matumizi ya dawa  za presha na moyo yataisha pale ambaapo uhai wa muhusika utafika mwisho hapa Duniani.

“Wakati mwingine tunachokifanya presha ikishuka tunapunguza dozi au kuondoa baadhi ya dawa ili mgonjwa apate dawa inayoendana na presha yake hivyo kazi yetu ni kurekebisha tu na sio mgonjwa kuacha kutumia dawa kabisa,”anaeleza Dk Rweyemamu.

LISHE KWA WAGONJWA

Husna Faraji ni  Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI)anasema kuwa katika lishe wanatazama mambo mbalimbali ambayo wanaweza kubaini kama muhusika analishe bora.

 “Tunahitaji jamii ielewe kuwa tunapozungumzia ulaji  usiofaa ni kutokuzingia makundi ya chakula na kiasi cha makundi ya chakula, tunasisitiza aina ya makundi ya chakula iliyopo lakini kingine ni kula makundi ya chakula kwa kuzingatia uwiano uliosahihi.

“Ulaji wa mboga za majani ni muhimu zaidi  kutokana na faida nyingi  za kiafya zinazopatikana  lakini  tunashauri kiwango cha mafuta na aina ya mafuta yanayotumika katika vyakula.

“Ushauri ni kuwa ni bora watu wakatumia mafuta ya mimea badala ya wanyama,hii ni kwasababu mafuta yanayotokana na wanyama yana ‘cholesterol’ mbaya ambazo zinahusishwa na matatizo ya moyo kwani  huziba mishipa ya damu  kwenye moyo hivyo   kuongeza nafasi ya kuweza kupata presha ya kupanda,”anafafanua. 

Husna anasema  matumizi ya vyakula vinayosindikwa viwandani ni hatari moja wapo kwa mtu kupata presha na magonjwa ya moyo.

“Matumizi ya vinywaji kama soda ambazo utayarishaji wake huwa unaviwango vikubwa vya sukari hii hupelekea shida katika afya ya moyo, tunashauri watu kupendelea vinywaji  yenye virutubisho  zaidi kama maziwa ,juisi ya matunda ,maji safi na salama  kuliko kutumia viwanywaji amabavyo vinasindikwa kwa muda mrefu kwa sukari na chemikali,”aanasema Husna.

Anasisitiza watu kupunguza ulaji wa vyakula yenye wanga  kutokana na aina hivyo ya vyakula kuweza kusababisha matatizo ya moyo

“Wanga inaongeza uzito  hali hiyo inaongeza nafasi ya kupata presha ya juu na matatizo ya moyo  magonjwa mengine yasiyo ya kuambukizwa kama kisukari kansa na mengineyo.

“Lakini pia tunasisitiza ufanyaji wa mazoezi kwasababu mtu anayefanya mazoezi tafiti zinaonesha huwa na uwezo wa kupunguza  nafasi ya kupata magonjwa hivyo nashauri  hasa tunapokuwa na uzito uliokithiri tuwe na ratiba ya mazoezi kila siku,”anashauri Husna.

Mwishooooo…..