January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jeshi la polisi,TCRA washirikiana kudhibiti utapeli mtandaoni

Na Doreen Aloyce, Timesmajira Online,Dodoma

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) na Jeshi la Polisi,wamekuwa wakishirikiana katika kuhakikisha wanadhibiti utapeli na wizi kwa njia ya mtandao

Ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti watoa huduma kwa kuhakikisha wanafuata miongozo ya kusajili na kuhakiki laini za simu huku wale wanao husika na uhalifu wa kuwaibia watu kwa njia hiyo ya mtandao wakichukuliawa hatua za kisheria.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa umma TCRA Lucy Mbogoro wakati akizungumza na waandishi wa habari Bungeni jijini Dodoma katika maonesho ya banda la taasisi hiyo yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia.

Lucy amesema kuwa tangu kukamilika kwa zoezi la uhakiki na usajili laini za simu Aprili 13,2023,wamefanikiwa kudhibiti wizi huku wale wote wanaofanya uhalifu mtandaoni watakamatwa.

“Katika kudhibiti utapeli kwa njia ya mtandao TCRA tumeendelea kutoa elimu kwa jamii namna ya kuwagundua jambo ambalo limesaidia kupungua kwa idadi ya mapateli hao,”amesema Lucy.

Sanjari na hayo akizungumza kuhusu usafirishaji wa vifurushi na vipeto Lucy amesema kuwa ili wananchi waepuke kutapeliwa na kupoteza bidhaa zao ni vyema wananchi wakatumia watoa huduma waliosajiliwa na TCRA.

Akisisitiza kuwa kuhusu kutuma vitu ambavyo ni hatarishi na hatari amesema TCRA imekua ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha mzigo unaosafirishwa hauna athari kwa wengine kama anavyoeleza.

Ikumbukwe kuwa TCRA ni taasisi ya serikali yenye majukumu ya kusimamia sekta za mawasiliano na utangazaji ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2003 ili kusimamia huduma za kielektroniki na posta na masafa ya mawasiliano nchini Tanzania.