Na Joyce Kasiki,Dodoma
MKUU wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Nchini Jenerali Venance Mabeyo ameliagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuendelea kubuni miradi ya maendeleo nchini kwani imelenga kulisaidia Jeshi hilo na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati akizindua Kituo cha burudani cha Medeli East ambacho kina ukumbi mkubwa, eneo la huduma ya chakula na michezo ya watoto Jenerali Mabeyo amesema, mradi huo ni muhimu kwa jeshi hilo hivyo ni vema wakaendelea kuwa wabunifu ili wajitegemee.
Amesema,hakuna haja ya kulalamika wakati kuna fursa ambazo zinataka ubunifu tu katika kubuni miradi itakayoliinua Jeshi hilo kiuchumi na kulifanya lijitegemee.
“Hakuna haja ya kuendelea kulalamika wakati fursa zipo, tuzitafute na tuzitengeneze zinaweza kujitokeza, lakini ukisubiri fursa zitengenezwe na mwingine wewe ukazichukue unakuwa mhalifu na mhalifu.”Alisema Jenerali Mabeyo na kuongeza kuwa
“Jeshi lina ardhi kubwa ambayo inatakiwa kujifikiria nini cha kufanya ambacho kitawapatia fedha.
Amesema wameanza na miradi midogo ndani ya vikosi vya Jeshi lakini watakuwa na miradi mikubwa ndani ya Jeshi na kwamba majeshi duniani yameendelea kwasababu ya kutumia ubunifu.
Kwa upande wa kituo hicho burudani, Jenerali Mabeyo aliwataka viongozi wa jeshi hilo kuendelea kukitunza na kukiboresha ili kushindana kibiashara kwa kutoa huduma bora.
“Huduma bora pekee yake ndizo zitakazosaidia kupata wateja wa kutosha kama huduma zenu zikiwa ovyo ovyo watu watakimbia wataenda sehemu nyingine,”amesema
Amesema na jambo hilo linahitaji ubunifu kufikiria huduma gani waboreshe ili kuwavuta watu kuja katika eneo hilo.
Pia alitaka kituo hicho kuwa mfano na chachu kwa wakuu wengine wa vikosi nchini kuwa na maono ya kuanzisha miradi kwa lengo la kuongeza uwezo wa kujiendesha wenyewe.
Kwa upande wake Mkuu wa Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema ukumbi huo unachukua watu kati ya 1,000 hadi 1,200 kwa wakati mmoja, ukumbi mdogo, jengo la utawala, ukumbi wa watu maarufu, eneo la huduma ya chakula na eneo la michezo kwa watoto.
Amesema mara baada ya uzinduzi wataanza kupokea oda kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kwamba ukumbi huo utatumika kwa shughuli za kijeshi pamoja na za kijamii.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja