May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Makalla na bodaboda mambo safi

Na Mwandishi wetu, TimesMajiraOnline

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla ametoa muda wa Miezi mitatu kwa Shirikisho la Vyama vya waendesha Bodaboda Jijini humo kuweka Mpango kazi kuwapanga vizuri Bodaboda ikiwa ni pamoja na utaratibu rasmi wa kuingia mjini na kutoka ili kuondoa hali uholela wa kuingia mjini unayoendelea kwa Sasa.

RC Makalla ametoa maazimio hayo wakati wa kikao Cha pamoja baina ya Viongozi wa Bodaboda, Jeshi la Polisi, LATRA, TARURA na TANROAD kilicholenga kujadili zuio la Bodaboda kuingia mjini lililokuwa limetolewa na Jeshi la Polisi.

Miongoni mwa maazimio yaliyotolewa na kikao hicho na yanapaswa kufanyiwa kazi na Kamati iliyoundwa ni pamoja na shughuli za Bodaboda kufanyika sambamba na kulinda taswira ya Jiji, Uwepo wa vituo rasmi vya Bodaboda vinavyotambulika, Uvaaji wa Sare, Kofia ngumu pamoja na Bodaboda kuwa sehemu ya kuwafichua wahalifu.

Aidha RC Makalla amesema baada ya kupatiwa Mapendekezo ya Kamati atahitisha kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ili kuweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha suala la kuingia mjini linafanyika kwa kuzingatia taratibu.

Hata hivyo RC Makalla amesema Serikali ya awamu ya sita Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inathamini kazi ya Bodaboda Kutokana na shughuli hiyo kutoa ajira kwa idadi kubwa ya Vijana.

Nao baadhi ya Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya waendesha Bodaboda akiwemo Said Kagomba ambae ndio Mwenyekiti wa Shirikisho ameishukuru Serikali kwa kukaa meza moja na Shirikisho Kuangalia namna Bora ya kushughulikia Jambo hilo na wameahidi kushirikiana na Serikali kuweka mazingira Bora ya biashara hiyo ili Bodaboda wa Dar es salaam wawe mfano mzuri wa kuigwa.