Na Lubango Mleka,Timesmajira Online
KILA mwaka Dunia huadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika (Day of the African Child) ni siku inayosherehekewa kila ifikapo Juni 16 ya kila mwaka tangu mwaka 1991 ilipoteuliwa na Umoja wa Afrika.
Ikiwa ni kuenzi michango ya watoto walioshiriki katika maandamano kwenye mji wa Soweto, Afrika Kusini mwaka 1976 pamoja na kujengea jamii uelewa juu ya umuhimu wa elimu bora na malezi kwa watoto.
Itakumbukwa kuwa, Juni 16, 1976, maelfu ya watoto katika nchi ya Afrika Kusini walikusanyika katika mji wa Soweto kwa ajili ya maandamano yenye malengo ya kudai elimu bora ambapo mamia ya watoto hao walipigwa risasi na kuuliwa na watoto zaidi ya 1000 walijeruhiwa.
Hivyo kila ifikapo Juni 16 ya kila mwaka, mataifa, jumuiya mbalimbali na jumuiya za kimataifa pamoja na wadau mbalimbali hukusanyika pamoja kwa ajili ya kujadili fursa na changamoto zinazowakumba watoto katika Bara la Afrika.
Kwa mwaka huu katika kuadhimisha siku hii, wazazi,walezi na wananchi mkoani Tabora wametakiwa kuacha kuwaficha na kuwatenga watoto wenye changamoto ya afya ya akili badala yake watenge muda wa kuwajumuisha na kuonana na wataalamu ili wapatiwe elimu jinsi ya kuishi na kuwalea watoto hao.
Hayo yamesema na Mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali la Akili Platform Tanzania mkoani Tabora linalojishughulisha na utoaji wa huduma kwa watoto wenye changamoto ya afya ya akili, Roghat Robert katika hafla ya kushiriki siku ya Mtoto wa Afrika iliyoandaliwa na shirika hilo Tabora Mjini.
Amesema kuwa, wapo baadhi ya wazazi ambao wamekuwa wakiwatenganisha watoto hao na wenzao kutokana na matatizo hayo.
Hivyo amewaomba wazazi na walezi wa watoto hao kuwasiliana na wataalamu wa afya ya akili jinsi ya kuwalea watoto wao.
” Tunawaomba wazazi,walezi, ndugu,jamaa na marafiki watambue kwamba changamoto ya afya ya akili ni suala mtambuka, kila mmoja anatakiwa kuwa balozi wa kulinda, kutetea, kuendeleza na kuimarisha suala la afya ya akili katika familia, kuwapeleka watoto hao kujumuika na watoto wengine ili waweze kuchangamana, kufanya shughuli za pamoja kulingana na hali walizonazo,” amesema Robert.
Ameongeza kuwa,wazazi watenge muda wa kuonana na wanasaikolojia kuongea nao kulingana na tabia za watoto wao wanazokuwa wanazifanya na kuzionesha katika familia zao.
Hali hii itasaidia kwa namna moja ama nyingine mzazi kutambua nini mtoto anahitaji na kwa wakati gani.
Aidha, amebainisha kuwa, kuna mitazamo mingi katika jamii juu ya watoto hao, ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakiona ni laana na mkosi katika familia, hivyo amewataka kuwaona kama watoto wengine wasiyo na changamoto ya afya ya akili.
“Mtoto aliyezaliwa na shida ya afya ya akili, wengine watasema amerogwa, ni laana na vitu kama hivyo, lakini ni kwamba hawana elimu ya kutosha juu ya mtazamo huo, ndiyo maana kwenye saikolojia tunasema ukiona mtu anamcheka mtoto mwenye tatizo la akili anayefanya matendo yake, huyo anayecheka ndio anatatizo,” amesema Robert.
Robert ameendelea kwa kusema kuwac mtazamo huo upo na ndio maana wanawaunganisha katika siku kubwa kama hiyo wazazi ili kuona kuwa siyo yeye pekee ndio mwenye mtoto ambaye ana changamoto hiyo kumbe wapo wengi.
Hata hivyo amebainisha changamoto zinazolikabili shirika la Akili Platform, kuwa ni uhaba wa viti mwendo, vifaa vya mawasiliano na wazazi kama vile simu janja zitakazo ungwa na mfumo wa kuonana na wataalamu moja kwa moja kama kuna shida kwa mtoto.
Pia vifaa vya ofisini, vifaa vya michezo kwa watoto hao, hivyo amewaomba wadau wote nchini kusaidia shirika hilo vifaa vitakavyo wezesha watoto hao kushiriki shughuli kama hizo na watoto wengine.
Kwa upande wake, Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete, Marcela Sila  wamelishukuru shirika la Akili Platform Tanzania na kuomba kuendelea na moyo wa kujitoa katika kusaidia watu wenye ulemavu wa akili.
“Kwanza kabisa natoa shukrani kwa niaba ya Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tabora Kitete, kwa kutuona na kuja kujumuika nasi kwa hiki kidogo mlichotupatia katika siku hii ya Mtoto wa Afrika, sisi tuko tayari kuendelea kuimarisha ushirikiano ili kuona namna ya kuisaidia jamii katika eneo la afya ya akili,” amesema Sila.
Naye Mratibu wa afya ya Akili Mkoa wa Tabora Dokta Swaumu Kimaro amesema kuwa anaendeleza ushirikiano na mshikamano katika kuhakikisha elimu ya afya ya akili inafika kila mtaa kwa Mkoa mzima wa Tabora kupitia wadau na kitengo chake.
Ambapo amewaomba wadau waweze kuwezesha shirika la Akili Platform Tanzania kwani linafanya kazi kubwa ya kizalendo kwa kujitolea.
Baadhi ya wazazi wa watoto wenye changamoto ya afya ya akili akiwemo Selina Laurent ameeleza kuwa baadhi ya changamoto zinazowakabili katika kuwalea watoto hao ni pamoja ukosefu wa usafiri unaowezesha kufika shuleni, unyanyaswaji kutoka kwa walimu na jamii na kukosekana kwa vifaa saidizi kama viti mwendo.
“Changamoto tunazozipata ni nyingi, hasa suala zima la unyanyapaa, watoto wetu wananyanyapaliwa sana hata shuleni wanasema mimi siwezi kumfundisha mtoto huyu amenishinda tafuta shule nyingine, unyanyapaa mwingine ni unakuta mtu hajui huyu mtoto yupo vipi akikosa anampiga badala ya kumuelekeza,” amesema Selina.
Huku Felister Masele,ametoa ushauri kwa wazazi kutowaficha watoto hao, kwani kufanya hivyo ni kuwanyima kufikia ndoto zao na kuonesha vipaji vyao kwa jamii.
“Mazingira ninayoishi siyo rafiki mimi nina mtoto wa kike mwenye tatizo la afya ya akili, jamii kubwa inayotuzunguka ni vijana wa kiume, sasa nina kuwa na wasiwasi mkubwa sana juu ya mtoto wangu,” amesema Felista Masele.
Shirika la Akili Platform Tanzania mkoani Tabora, limeadhimisha siku hii ya Mtoto wa Afrika, ambayo kwa mwaka huu inakauli mbiu isemayo “Zingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa kidigitali”.
Kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji wa maziwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete katika kitengo cha watoto wenye matatizo ya afya ya akili, kufanya michezo mbalimbali kwa watoto hao, pamoja na mjadala unaolenga namna ya kusaidia wazazi na watoto wanaopelekewa na changamoto kama hizi.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia