Na George Mwigulu,Katavi
Wakazi wa Mkoa wa Katavi wametakiwa kuondokana na fikra potofu kuwa ugonjwa wa kipindupindu husababishwa na kulogwa, badala yake wazingatie kanuni za afya, kwani ugonjwa huo unaepukika.
Ushauri huo umetolewa kufuatia jamii mkoani hapa hasa kwa wakazi wa vijijini wanapoishi wakulima na wafungaji kujihusisha vitendo vya kulipiza visasi na kusababisha vifo vya watu wengine, baada ya kwenda kwa waganga wa kienyeji kupiga ramli ambazo ni choganishi wanapougua magonjwa ikiwemo kipindupindu, wakidhania wamelongwa.
Rai hiyo imetolewa jana na mratibu wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko wa Hosptali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, Dkt. Taphinez Machibya, alipokuwa akizungumza na Majira ofisini kwake kuhusiana na magonjwa ya mlipuko.
Amesema jamii isipotambua maana ya ugonjwa wa kipindupindu,chanzo chake, dalili zake na athari zake na kushindwa kuchukua hatua ya kuudhibiti wataendelea kuathirika na wengine kupoteza maisha.
Dkt Machibya amesema ugonjwa wa kipindupindu kitaalumu husababishwa na aina ya bakteria ambao wapo kwenye mazingira tunayoishi.
Amesema bakteria hao wanapoingia kwenye mwili wa binadamu hukaa kwenye mfumo wa chakula (utumbo) na kuleta athari kubwa. Amefafanua kuwa mabaki ya matapishi au kinyesi yanayobaki yakiguswa na mtu mwingine au yakachukuliwa na nzi kutoka eneo moja hadi jingine, hasa kwa kugusa vyombo vya maji, chakula, chakula chenyewe au mtu mwenyewe akagusa mgonjwa atakuwa kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa.
Ameweka wazi kuwa ugonjwa wa kipindupindu unaweza kutokea kwa kutupa takataka hovyo, kuiva matunda mengi pamoja na kujisaidia nje ya mashimo ya vyoo hasa kwenye mikusanyiko ya watu wengi.
Hivyo amewataka wananchi kujenga vyoo na kuvitumia kwa usahihi. Dkt Machibya amewaambia wananchi kuwa pindi watakapoona dalili za homa, kutapika, uchovu na kuharisha majimaji ya rangi inayofanana na maji yaliyoosha mchele inawapasa kutoa taarifa kwenye vituo vya afya ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Aidha amesema jamii inapaswa kutambua athari zinazoweza kutokea kwa kusababishwa kipindupindu ambazo ni vifo ndani ya muda mfupi na taifa kupoteza rasilimali watu,familia kuwa na mzingo wa kuelea watoto yatima waliofiwa na wazazi wao.
Athari nyingine kwa mujibu wa mratibu huyo ni upotevu wa rasilimali fedha kwa sababu ni ugonjwa ambao unahitaji mapambano makali ndani ya muda mfupi, kwa hiyo jamii na Serikali kutumia bajeti kubwa ili kuzuia kasi ya maabukizi.
Hivyo ameitaka jamii kwa ujumla kuzingatia taratibu za usafi kwenye makazi yao pamoja na kuhifadhi vizuri taka mwili hasa taka zitokanazo na choo na kunawa mikono kwa maji safi na salama na wala sio kuwa na dhana potofu za imani za kishirikina.
Mmoja wa wananchi wa mkoa huo, Alex Mwandu mkazi wa mtaa wa Nsemlwa amesema Serikali inapaswa kutoa zaidi elimu ya magonjwa ya mlipoko.
Mwandu ameongeza kuwa elima kama itatolewa kwenye jamii hasa ya vijijini itasaidia watu kuchukua tahadhari na kujilinda dhidi ya ugonjwa huo na kuachana na imani potofu za kuhusu magonjwa huo.
Naye Aisha Hassain Mkazi wa mtaa wa Misukumilo Manispaa ya Mpanda mkoani humo amesema uwepo wa ongezeko la vituo vya afya na zahanati vijijini itasaidia kutokomeza magonjwa ya mlipuko kwenye jamii.
More Stories
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia