May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yaaswa kuwatunza watoto Yatima

Na Queen Lema,Arusha

Jamii imeaswa kuacha Tabia ya kuwapeleka watoto ambao wamefiwa na wazazi wao kwenye vituo vya kule watoto Yatima na badala yake wawatunze ikiwa ni pamoja na kuwapa mahitaji muhimu ya kila siku.

Endapo kama jamii itaweza kuwasaidia watoto hao kwa njia hiyo basi kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani ambao wanatokana na kukosa baba na mama.

Hayo yameelezwa Leo na Wakili Mary Mwita ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha kisheria kijulikanacho kama Smart Community on legal Protection wakati akikabidhi misaada mbalimbali kwa watoto wa kituo cha watoto yatima Cha Ungalimited Kinachomilikiwa na kanisa la International Evangelism church Jijini Arusha.

Wakili Mary amesema kuwa jamii kwa sasa inatakiwa ihakikishe kuwa mahitaji ya watoto hasa Yale ambayo ni muhimu wanapata hata kama wazazi wao hawapo tena duniani

Amefafanua kuwa wazazi wanapotwaliwa na Mungu waliobaki wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanawatunza na kuwajali watoto hata kama sio wao

“Tukifanya hivyo ni wazi kuwa idadi ya watoto ambao wanaletwa kwenye vituo itapungua kwa kiwango kikubwa ,ebu sasa kila mtu aone kuwa mtoto wa mwenzako ni wako na una jukumu kubwa sana la kuweza kumlinda mpaka afike umri wa kujitegemea,”amesema.

Wakati huo huo alitoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa wanajijengea tabia ya kuwatembelea watoto wenye maitaji maalumu pamoja na watoto wao ili kuweza kupandikiza mbegu ya amani na upendo .

“Leo nimefuatana na timu kubwa sana ya watoto ambapo napenda kupandikiza mbegu ya upendo na wajue na kutambua kuwa hili la kuangalia mayatima na wenye mahitaji maalumu ni sehemu ya maisha yao”ameswma

Akiongea kwa niaba ya watoto ambao waliofia kituoni hapo kwa ajili ya kutoa misaada,Faith ole Ngereza amesema kuwa hata watoto wengine wanapaswa kutambua kuwa mayatima ni sehemu ya jamii.

Faith amebainisha kuwa yatima wanahitaji misaada mkubwa na hawatakiwi kuachwa wakiwa na shida kwa kuwa hata mandiko matakatifu yanasisitiza jamii kuweza kuwajali yatima.

Hata hivyo misaada iliyotolewa ni pamoja na vifaa vya shule,pamoja na zawadi mbalimbali ambapo baada ya kukabidhiwa kwa misaada hiyo watoto wa kituo hicho kwa kushirikiana na wageni waliweza kushiriki katika michezo mbalimbali.