NA
K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, KIGOMA
JAJI
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamisi Juma, amesema Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema lengo la vyombo vyote vya dola ni
ustawi wa wananchi.
Mhe.
Jaji Mkuu, ameyasema hayo mjini Kigoma Aprili 19, 2024, wakati akifungua Kikao Kazi kati ya Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi (WCF), Mahakama ya Tanzania na Watendaji wa Tume ya Usuluhishi na
Uamuzi (CMA) mjini Kigoma lengo kuu likiwa ni kujenga uelewa wa Sheria ya Fidia
kwa Wafanyakazi.
“WCF
ni Mfuko unaogusa ustawi wa wananchi, kwasababu unaweza kuwa unamtegemea mama,
kaka, bahati mbaya akapata ajali akafariki, hapa ustawi wa familia unaweza
kutoweka, kama hakuna Mfuko unaoweza kubeba hilo jukumu, kwa hivyo huu Mfuko ni
muhimu mno mno.” Amebainisha Mhe. Profesa Juma.
Aidha
Mhe. Profesa Juma amehimiza umakini na uadilifu katika utekelezaji wa sheria
hiyo ya Fidia kwa Wafanyakazi.
“Ukosefu
wa umakini, udanganyifu vyote vimechangia kuua mifuko ambayo ilikuwa na malengo
mazuri sana. Tusipokuwa waangalifu, mfuko huu wa WCF vile vile unaweza
kukumbana na tatizo hili. Tukielewa vizuri mantiki ya kuanzishwa mfuko huu tutaufanya
uwe endelevu na himilivu,” amesema.
Aidha
Mhe. Jaji Mkuu ameipongeza WCF kwa kupiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA
katika utekelezaji wa majukumu yake na kukumbusha umuhimu wa mifumo ya taasisi
za umma kusomana ili kurahisisha utoaji wa huduma.
“Ifike
mahala mfanyakazi anapowasilisha madai yake WCF, mfumo mzima uwe unaelewa
kwamba mfanyakazi fulani amepata ajali kazini au amefariki. Mifumo ya serikali ikiweza
kutambuana pia itasaidia sana kuziba mianya ya udanganyifu.” Alisisitiza.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw.
Emmanuel Humba, amemuhakikishia Mhe. Jaji Mkuu kwamba Mfuko unaendeshwa kwa
ufanisi mkubwa na umepata mafanikio makubwa katika kutekeleza malengo yake.
“Malipo
ya fidia kwa Wafanyakazi yameongeza kutoka TZS 3.88 bilioni Kwa mwaka 2016/2017
hadi kufikia TZS 23.58 bilioni kwa mwaka 2022/2023. Hili ni ongezeko kubwa la
malipo ya fidia kulinganisha na kiasi cha TZS 250 milioni zilizokuwa zikilipwa
na Waajiri kwa mwaka kabla ya kuanza Mfuko.” Amefafanua Bw. Humba.
Aidha,
michango ya Waajiri iliyokusanywa imeongezeka kutoka TZS 68.40 bilioni Kwa
mwaka 2015/2016 hadi kufikia TZS 86. 48 bilioni kwa mwaka 2022/2023, amesema
Bw. Humba.
“Faida
inayotokana na uwekezaji ya fedha zilizobaki baada ya kulipa mafao imeongezeka
kutoka TZS 1.60 bilioni Kwa mwaka 2015/2016 hadi kufikia TZS 102.43 bilioni kwa
mwaka 2022/2023, lakini pia thamani ya
Mfuko imeongezeka kutoka TZS 65.68 bilioni Kwa mwaka 2015/2016 hadi kufikia TZS
602.78 bilioni kwa mwaka 2022/2023.” Amefafanua.
Kuhusu
ustahamilivu wa Mfuko katika kutekeleza majukumu yake, Mwenyekiti huyo wa Bodi
amesema kuwa tathmnini ya uhai na uendelevu wa Mfuko iliofanywa na Shirika la
Kazi Duniani (ILO) inaonesha kwamba Mfuko unauhimilivu (Sustainability) kwa
kipindi cha miaka 30 kuanzia mwaka wa tathmini 2022/2023.
Akizungumzia
kuhusu nia ya kikao kazi hicho, Bw. Humba alibainisha kuwa pamoja na kwamba
jukumu la kulipa fidia limekasimiwa kwenye Mfuko, Sheria ya Fidia kwa
Wafanyakazi imeweka utaratibu na vyombo vya kushughulikia madai ya wanufaika
pale wanapokuwa hawajaridhika na fidia iliyolipwa au maamuzi ya Mfuko
yanayokinzana na matarajio yao.
Akifafanua
zaisdi alisema, Sheria inamtambua Waziri Mwenye dhamana ya masuala ya kazi kuwa
ni Mamlaka ya kwanza ya rufaa dhidi ya uamuzi wa Mfuko na Mahakama Kuu
Divisheni ya Kazi kuwa Mamlaka ya mwisho ya rufaa.
“Kutokana
na hitaji hili muhimu la kisheria, Bodi ya Wadhamini ya WCF, Menejimenti ya
Mfuko pamoja na Watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi waliona kuna hitaji
la kufanya vikao kazi kwa lengo la kubadilisha uzoefu, kujenga uelewa wa pamoja
na kubainisha maeneo ya sheria yanayohitaji maboresho kwa lengo la kuongeza
ufanisi katika kutekeleza Sheria hiyo.” Alisema.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John
Mduma ameeleza kuwa ushirikiano baina ya Mfuko na Mahakama ni muhimu kwa vile
kuna maeneo mengi ambayo Mfuko unakutana na Mahakama katika utekelezaji wa
majukumu yake.
“Sisi
kama WCF shughuli zetu hazikamiliki bila ya uwepo wa shughuli za Mahakama. Kwa
mfano katika kushughulikia masuala yanayohusu mirathi, Mfuko hutegemea maamuzi
ya Mahakama.” Alisema Dkt. Mduma.
Awali,
akizungumza kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu kufungua Kikao Kazi hicho, Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambia
alisema kuwa kumekuwa na vikao kazi vitano ambavyo vimefanyika baina ya
Mahakama, WCF na Watendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) huko Bagamoyo, Mwanza, Arusha, Songea na Kigoma.
Alibainisha
kuwa jumla ya Viongozi na watumishi 290 wameshiriki katika Vikao Kazi hivyo,
wakiwemo Majaji 70, Naibu Wasajili 33, Watendaji 11, Wadau 48, Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi 32 na zaidi ya watumishi wa Mahakama 96.
JAJI Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamisi Juma, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi baina ya WCF, Mahakama na CMA mjini Kigoma Aprili 19, 2024
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria