April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jafo azindua mradi wa twiga wa kijani


Na Daud Magesa, Timesmajira Online Mwanza


WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira,Selemani Jafo, ameziagiza halmashauri zote nchini kupanda miti na maua pembezoni mwa barabara ili kupendezesha Miji na kutunza mazingira.

Ambapo amesema agenda ya usafi haipendezi kuona Jjiji au Manispaa uchafu umetapaa katika mitaro,mvua zikinyesha inaziba na kusababisha miundombinu kuharibika,hivyo halmashauri zote zihakikishe zinazipatia zabuni kampuni zenye uwezo wa kukusanya na kuondosha taka ili miji iwe safi.

Jafo ameagiza hayo Machi 28,2024 wakati akizindua kampeni ya Twiga wa Kijani katika shule ya msingi Jeshini,wilayani Ilemela mkoani Mwanza inayolenga kupata miti 6,000 katika shule 30 za msingi na 30 za sekondari huku ameeleza kuwa itahamasisha wananchi kutunza mazingira.

“Miji inatia aibu, uchafu umetapakaa,mitaro ya maji inaziba sababu ya uchafu na miundombinu inaharibika. Halmashauri kwa nini hamfanyi beutification katika maeneo yenu? Hakikisheni mnapanda miti mizuri ya kupendezesha na kuvutia miji pembeni mwa barabara ili wageni wakifika waone madhari ya miji yetu,”amesema Jafo.

Pia ameeleza kuwa kutokana na taifa kukabiliana mabadiliko ya tabianchi,ukame na mvua zisizo na mpangilio,agenda ya kutunza mazingira haina mjadala na kuzitaka kampuni na taasisi kupanda miti na kutunza mazingira ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Jafo amesema elimu ya mazingira iko chini hivyo shirika la Wezesha Binti na Mama Mjasiriamali (WBM)kujitosa kupandikiza agenda hiyo kwa watoto kupanda miti shuleni itasaidia kutunza mazingira na mradi huo wa Twiga wa Kijani haukuja bahati mbaya.

“WBM na TFS shirikianeni kuanzisha vitalu vya miti shuleni visaidie wananchi wa maeneo jirani,halmashauri zitenge bajeti ya kustawisha miche zipande miti milioni 1.5 kwa mwaka,zikifanya hivyo tutafika mahali sahihi,”.

Amesema kampuni nyingi zinazalisha hewa ukaa na kusababisha athari za mazingira yaige mfano wa ATCL na kuzitaka kampuni zinazozalisha nishati safi ya kupikia kuunga mkono juhudi za serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo kwa jamii kuachana na kuni na mkaa ili kuokoa miti inayokatwa.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya Sengerema,Senyi Ngaga,amesema kutokana na idadi kubwa ya watu mkoani humo na ukuaji kiuchumi suala la kutunza mazingira ni muhimu.

“Mazingira yasipotunzwa tutahatarisha uhai wetu na viumbe vingine,ni muhimu kupanda miti ili kuunga mkono juhudi za Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla licha ya changamoto ya kubadili mitizamo ya watu,”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL,Mhandisi Ladislaus Matindi amesema,usafiri wa anga unachangia uchafuzi wa mazingira kwa kuzalisha hewa ukaa kwa asilimia 2.4 hadi 2.5 na takwimu zinaonesha ifikapo mwaka 2050 kiwango cha jotogesi na uharibifu wa mazingira kidunia kitafikia asilimia tano.

Amesema wamekubaliana na Jumuiya ya Usafiri wa Anga kutumia injini (Smart) zinazotumia nishati mbadala ya nafaka ( mahindi na jamii ya maharage),badala ya petrol ili kupunguza ongezeko la uchafuzi na kusaidia sekta binafsi kupunguza hewa ukaa katika anga.

Pia,kuhakikisha ndege hazichangii uharibifu wa mazingira kwa kuzalisha hewa ukaa,watapunguza muda wa ndege kukaa angani na kuboresha njia maalumu ili kupunguza gesijoto inayosababishwa na moshi unatokana na kuungua kwa mafuta ya petroli.

Awali Mkurugenzi wa WBM,Latifa Mohamed amesema kampeni hiyo itapunguza athari za mazingira na kuleta maendeleo chanya na endelevu kwa jamii,katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuwawezesha wanawake na mabinti kuondokana na changamoto hiyo na kujiingizia kipato.

Latifa amesema mradi huo ni endelevu wenye kaulimbiu,’Mazingira yetu, Maisha yetu,’ utasaidia kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira kwa kutoa elimu endelevu ya uhifadhi mazingira kwa wanafunzi na kutangaza bidhaa za ATCL,utatekelezwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza,Mtwara,Mbeya,Kagera na Kilimanjaro.