Na Lulu Mussa,TimesMajira online,Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo amezitaka asasi zisizo za Kiserikali/Asasi za Kiraia (NGOs, CBOs na CSOs) zinazojihusisha na shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini kushiriki kikamilifu katika kusukuma mbele ajenda ya Mazingira Nchini.
Waziri Jafo ameyasema hayo hii leo katika kikao maalumu kilichofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma kilichojadili mchango na majukumu ya Asasi zisizo ya Kiserikali katika Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini.
Jafo amesema lengo la Serikali ni kuhamasisha utendaji kazi wa Asasi hizo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu stahiki na kuimarisha uratibu wa shughuli za Usimamizi wa Mazingira nchini na kudumisha mahusiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Asasi zisizo za Kiserikali zinazohusu Hifadhi ya Mazingira.
“Leo ni siku ya ndoto yangu kukutana na wadau muhimu katika kusukuma mbele agenda ya Mazingira, hii inanipa faraja kubwa kuona tunao wadau wengi sana wenye nia ya dhati katika kusukuma mbele agenda hii muhimu”
Jafo amesema bajeti ya Mazingira ni ndogo na kupitia wadau hao ametoa rai kwao kujikita zaidi katika usimamazi wa mazingira kwa kushirikiana na Serikali ili kuratibu shughuli za Mazingira kwa ufanisi zaidi katika Mikoa yote.
“Nafahamu, nyinyi mmekuwa wadau wakubwa katika hifadhi ya mazingira nchini na mmekuwa mkijitoa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu agenda hii muhimu ya mazingira kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo,” alisisitiza Waziri Jafo .
Waziri Jafo amezitaka asasi hizo kusogeza huduma katika maeneo mengi nchini ili kuleta tija na kupambana na uharibifu wa mazingira ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na shughuli za kibanadamu zisizo endelevu.
“Ndugu zangu hatuwezi kupata uchumi endelevu bila kudhibiti mazingira yetu, uharibifu wa mazingira duniani ni wakutisha, athari za mabadiliko ya tabianchi nsi kubwa na kumekuwa na ongezeko la kina cha maji katika Mito, Mabwawa na Maziwa kutokana kuongezeka kwa mvua juu ya wastani,” Jafo alisisitiza.
Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga alisema Serikali na Asasi za Kiraia zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja kwa kuzingatia misingi ya Uwazi, Uadilifu, Sera, Sheria, Taratibu na Miongozo ya Serikali inayolega kuongeza ufanisi, tija na uendelevu katika usimamizi wa mazingira nchini.
Mmoja wa washiriki wa Mkutano huo Bi. Winifrida Shonde kutoka Asasi ya Tanzania Environment and Empowerment Movement (TEEM) aliishauri Serikali kuhakikisha kila asasi za zisiso za kiraia kupewa majukumu ya kuainisha malengo katika katika hifadhi ya mazingira ili kuweka utaratibu bayana wa utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa mazingira hapa nchini.
Katika kikao hicho baina ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGOs, CSOs & CBOs) kimehusisha takribani washiriki Mia Mbili kutoka kote nchini.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini