May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya madaktari nchini Iran wakifurahia katika picha baada ya mafanikio makubwa ya vita dhidi ya COVID-19. Mpaka kufika ijumaa mchana, zaidi ya wagonjwa 66,500, walioambukizwa virusi vya COVID-19 nchini humo walikuwa wameruhusiwa toka katika hospitali mbalimbali nchini baada ya kupona

Iran yasisitiza ipo tayari kutoa msaada Marekani

TEHRAN, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kiislamu Iran, Dkt.Said Namaki amesema taifa lake lipo tayari kuisaidia Marekani kukabiliana na matatizo mbalimbali yakiwemo ya corona.

Aliyasema hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter wakati akijibu madai ya Waziri wa Afya wa Marekani ambaye alisema,Marekani ipo tayari kuisaidia Iran kupambana na corona.

Dkt.Namaki alisema,Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonesha kivitendo uwezo wake mkubwa wa kakabiliana na matatizo kama hayo ya corona na kuongeza kuwa, Tehran iko tayari kuwasaidia wananchi wa Marekani wanaoteseka kwa maradhi ya COVID-19 kwa sasa kutokana na uzembe wa serikali yao.

“Leo (hivi karibuni) Waziri wa Afya wa Marekani amedai katika kikao cha Shirika la Afya Duniani kwamba yuko tayari kuisaidia Iran kupambana na corona, lakini kama nilivyosema kwenye kikao hicho,

“katika kujibu madai hayo ya kipuuzi kwamba leo hii Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu imepata mafanikio makubwa na imekaribia kuudhibiti ugonjwa huo kwa ushirikiano wa wananchi na viongozi wao na katika kilele cha heshima na mafanikio ya kujivunia,”alidai.

Dkt.Namaki alisema,wakati ambapo dunia inaona jinsi Marekani ilivyoshindwa kuudhibiti ugonjwa huo, Iran iko tayari kuwasaidia wananchi wa Marekani wanaoteseka sana kwa janga hilo la corona.

Hivi karibuni Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, Tehran inatumia mbinu mpya kabisa za kukabiliana na corona na kwamba vipimo vinavyofanywa vya proteini mpya ijulikanayo kiutalamu kwa jina la ‘fungomwili’ (antibody) ni miongoni mwa mbinu hizo mpya zinazotumiwa na Iran kutambua wagonjwa wa COVID-19.

Hivi karibuni pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilizindua na kuonesha hadharani bidhaa mbalimbali za kiteknolojia za kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 ambazo zimeundwa na mashirika ya elimu-msingi ya Iran ambayo msingi wake ni elimu.

Miongoni mwa bidhaa hizo ni kifaa cha kupima haraka corona, kifaa cha ozonizer, lango maalumu lenye uwezo wa kupulizia dawa za kuua virusi kwenye magari yanayopita na pia kugundua kiwango cha joto kwa waliomo ndani ya gari,programu tumishi ya Tak inayohusu lishe na kinga ya corona pamoja na kifaa chenye uwezo wa kugundua mwili na sehemu kilipo kirusi cha corona katika umbali wa mita 100 kwa sekunde chache.

Aidha, kifaa hicho ambacho ni mara ya kwanza kabisa kuvumbuliwa duniani kimepewa jina la Musta’an 110, na kinaweza kugundua corona bila kuchukua vipimo vya damu.

Sherehe za uzinduzi wa kifaa hicho cha kipekee zilihudhuriwa na Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH.