Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Iwapo tutalitambua suala la kuasisi serikali ya Kiislamu nchini Iran kuwa lilipewa kipaumbele cha kwanza katika fikra za kisiasa za Imam Ruhullah Khomeini, basi hapana shaka kwamba suala la kukomboa Quds tukufu na ardhi za Palestina kwa ujumla kutoka kwenye mikono ya Wazayuni Maghasibu wa Israel lilipewa umuhimu mkubwa katika fikra na kazi za kisiasa za shakhsia huyo adhimu nje ya Iran.
Moja kati ya hitilafu za kimsingi za Imam Khomeini na utawala wa Kipahlavi wa Shah ilikuwa ni ushawishi wa Wazayuni ndani ya Iran na kuwepo Waisraeli katika nafasi za serikali ya wakati huo ya Shah. Kwa maneno mengine ni kuwa, tunaweza kusema kuwa suala la kukomboa taifa la Iran na taifa la Palestina lilikuwa jambo la dharura na lenye kipaumbele cha kwanza katika fikra za kimapinduzi za Imam Khomeini, jambo ambalo linadhihiri wazi zaidi katika maandiko, hotuba na mapambano yake ya kisiasa.
Katika ujumbe wake mashuhuri wa sikukuu ya Nouruzi ya mwaka 1341 Hijria Shamsia, unaosadifiana na mwaka 1962, Imam Khomeini alizungumzia mauaji yaliyofanywa na serikali ya Shah dhidi ya Waislamu na wanazuoni wa dini kwa ajili ya kulinda maslahi ya utawala haramu wa Israel nchini Iran. Tangu wakati huo, Imam alikuwa akizungumzia kadhia hiyo kwa nguvu zake zote katika minasaba mbalimbali ndani na nje ya Iran. Kwa mfano katika ujumbe wake kuhusu muswada wa jumuiya za kimkoa.
Moja ya misimamo mikali mno na imara ya kisiasa ya Imam Khomeini dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ni hotuba yake mashuhuri katika msikiti wa Aadham mjini Qum, Iran baada ya kuachiwa huru kutoka jela. Imam Ruhullah Khomeini alisema katika hotuba hiyo kwamba: Enyi wananchi! Dini yetu inatuamuru kuwapinga maadui wa Uislamu. Qur’ani inatutaka kutoungana na maadui wa Usilamu mkabala wa safu za Waislamu. Hakika taifa letu linapingana na Shah (mfalme wa Iran) katika kushikamana kwake na dola la Israel.
Upinzani wa Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ulipamba moto zaidi baada ya mauaji yaliyofanywa na utawala wa Shah katika chuo cha kidini cha Faidhiya mjini Qum. Imam alitoa hutuba kali na ya kihistoria kwa mnasaba huo akisisitiza juu ya kuendelezwa mapambano na kupinga ushawishi wa Wazayuni katika masuala ya Iran.
Tarehe 18 Agosti 1969 Wazayuni wa Israel waliuchoma moto msikiti wa al Aqsa. Imam Khomeini alilaani vikali kitendo hicho na akawataka Waislamu wasiujenge upya msikiti huo ili ubakie kama ushahidi wa jinai za Wazayuni mbele ya macho ya Waislamu hadi pale Palestina itakapokombolewa kikamilifu kutoka katika makucha ya Maghasibu..
Katika kipindi chote cha kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Imam Khomeini aliendelea kutoa taarifa mbalimbali, kujibu maswali ya maulamaa na kutoa fatuwa zinazowawajibisha Waislamu wote kupigana vita vya jihadi kwa ajili ya kuikomboa Palestina na kuyasaidia makundi ya mapambano ya Kipalestina. Imam Khomeini alihuisha tena maana ya jihadi na kupigania ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Kilele cha harakati za Imam za kupinga Uzayuni na kuunga mkono mapambano ya ukombozi wa Palestina kilikuwa ni kuainisha Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuikomboa Quds tukufu na kupambana na Wazayuni. Imam Ruhullah Khomeini alisema katika ujumbe wake kwa mnasaba huo kwamba: Siku ya Quds ni siku ya kimataifa. Si siku ya Quds pekee bali ni siku ya mapambano ya waliodhulumiwa dhidi ya mabeberu. Mataifa yote yanapawa kusimama kidete na kutupa kiini cha ufisadi katika kapu la taka. Siku ya Quds ni siku ya kufanya juhudi za kuikomboa Quds. Ni siku ya Uislamu na kuhuisha dini hiyo tukufu, na siku ya kutekeleza sheria za Kiislamu katika nchi za Waislamu. Siku ya Quds ni siku ya kutengana haki na batili”.
Imam Khomeini aliamini kwamba Uzayuni ni mwana wa ukoloni na ubeberu ambao daima unapewa himaya na misaada ya Marekani. Akiashiria uhusiano mkubwa wa Wazayuni na ubepari na mabepari wa nchi za Magharibi hususan Marekani, Imam Khomeini anaeleza chanzo na sababu ya kujitokeza Israel akisema: Israel iliundwa kutokana na njama na ushirikiano wa serikali za kikoloni za nchi za Magharibi na Mashariki kwa shabaha ya kuyakandamiza na kuyakoloni mataifa ya Kiislamu na hii leo inaungwa mkono na kusaidiwa na wakoloni wote. Uingereza na Marekani zimeuimarisha kijeshi na kisiasa utawala ghasibu wa Israel na kuuhamasisha dhidi ya Waarabu na Waislamu kwa kuupa silaha hatari za mauaji”.
Miongozi mwa sifa makhsusi za Uzayuni ambazo zinaonekana sana katika hotuba za Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ni aidiolojia yake ya “Kuanzia Nile Hadi Furati”. Imam alikuwa akiamini kamba uvamizi wa Israel dhidi ya nchi za Kiislamu hautaishia Palestina, Lebanon na katika miinuko ya Golan huko Syria, bali Wazayuni wanakusudia kuunda dola wanaloliita Israel Kuu na hatari yao inazilenga nchi zote za Kiislamu za Mashariki ya Kati. Imam alikuwa akizitahadharisha nchi za Kiarabu na kuziusia zijizatiti kwa silaha kwa ajili ya kutokomeza utawala huo bandia na ghasibu katika jiografia ya kisiasa na eneo la Mashariki ya Kati.
Imam Ruhullah Khomeini alikuwa akiamini kwamba serikali na makundi ya Kipalestina hayapaswi kupoteza wakati katika mijadala ya kidiplomasia kwa ajili ya kupata haki zilizoghusubiwa za wananchi wa Palestina. Aliamini kuwa njia pekee ya kumuangamiza adui ghasibu na Mzayuni ni mapambano ya silaha na vita vya jihadi. Imam Khomeini alikuwa akiamini kwamba utawala ghasibu wa Israel ni kama donda la saratani ambalo njia pekee ya kulitibu ni upasuaji, kulikata na kuling’oa kabisa. Imam alikuwa akiwalaumu watu wanaotumia mbinu za kisiasa kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kadhia ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na alikuwa akisema: Ninawausia viongozi wa Kipalestina waache kwenda huku na kule kukutana na Wazayuni na wapigane hadi tone la mwisho la damu zao. Wapalestina wanapaswa kumtegemea Mwenyezi Mungu, kwani kukutana na Wazayuni kunayavunja moyo mataifa ya wanapambano.
Imam Khomeini aliutambua mfarakano na hitilafu kuwa ndio tatizo kuu la Waislamu na nchi za Kiislamu pia na kwamba jambo hilo linawadhoofisha mno mkabala wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Imam Khomeini alikuwa akisema, “Lau Waislamu wataungana na kila mmoja wao akamwaga ndoo moja tu ya maji, basi utawala ghasibu wa Israel utaangamia”.
Imam Khomeini ametaja siri ya ushindi kuwa ni kupigana na kuwa tayari kuuawa shahidi na kulitaja suala hilo kuwa ni siri ya Qur’ani ambayo inamfikisha mwanadamu katika mafanikio zaidi na kutimiza matarajio ya mataifa bila ya kuzingatia maisha ya kimaada na kidunia. Imam Ruhullah Khomeini ametaja mapambano ya Intifadha ya Palestina na harakati ya Kiislamu na ya wananchi kuwa ni mti uliobarikiwa na nyota inayong’ara na kusisitiza kuwa mbinu hiyo ya mapambano ndiyo stratijia kamili zaidi kwa ajili ya kuuangamiza kikamilifu utawala ghasibu wa Israel.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia