November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yatazamia kukamilisha zoezi la anuani za makazi ndani ya siku 40

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala, amesema Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inatazamia kukamilisha zoezi la uwekaji anuani za makazi ndani ya siku 40.

Hivyo amewaomba wananchi wa Wilaya ya Ilemela, kutoa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo kwa urahisi.

Massala ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wilayani Ilemela mkoani Mwanza,ambapo amesema zoezi linaloendelea la uwekaji anuani za makazi kwa wananchi,Rais alitoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa kwa ajili ya kuwaelekeza kwamba zoezi la uwekaji wa anuani za makazi linafanyika nchi nzima.

Hivyo na wao kama Mkoa wa Mwanza kupitia Mkuu wa Mkoa Mhandisi Robert Gabriel,aliwaita na kuwapa maelekezo ya kuanza utekelezaji wa zoezi hilo.

Amesema,wanakusudia ndani ya siku zisizo zidi 40,Manispaa ya Ilemela wawe wamekamilisha zoezi la uwekaji anuani za makazi,ili kuendana na kasi na maagizo ya Rais Samia.

“Kwa Wilaya ya Ilemela sisi zoezi tuliisha lianza kitambo lakini kwa awamu ya pili, tumelianza siku ya tarehe 12, tunatazamia kuwa na nyumba 70,000, ambazo tunatazamia kuziwekea namba,mpaka sasa zoezi linaendelea vizuri tuna vijana ambao wanapita kwenye mitaa yetu,”amesema Massala.

Pia amesema wameisha fanya vikao na wenyeviti wa mitaa pamoja na viongozi mbalimbali ambao wapo kwenye mitaa yao, wanawapa ushirikiano.

“Nitumie fursa hii kuwahamasisha wananchi, tumeona baadhi ya maeneo watendaji wetu wamepata changamoto, kupitia waandishi wa habari nimeona tuendelee kutoa elimu kwa wananchi waelewe umuhimu wa kwanini tunaweka anuani za makazi,ambazo zipo katika hatua tatu,kwanza ni ya kuandika namba,lakini kuna ambao tayari wameanza kuingizwa kwenye mfumo,” amesema Massala.

Mbali na hayo Mkuu huyo wa Wilaya ya Ilemela Massala,ameelezea faida za zoezi la uwekaji anuani za makazi ni pamoja na kutambua maeneo yao kwa kutoa majina ya mitaa zoezi ambalo lina utaratibu tayari viongozi wa mitaa wameisha elekezwa.

Amesema,wakisha itambua mitaa,itawapa faida kubwa ya kuelekeza watu wanaotaka kufahamu nani ana kaa wapi, kupeleka mizigo pia kutuma vifurushi mbalimbali litakuwa ni jambo ambalo limerahisishwa kwa njia hiyo katika suala la ulinzi na usalama nayo ni faida kubwa ambayo wananchi wataipata.

“Kwaio nitumie nafasi hii niendelee kuwaomba wananchi wetu wa Wilaya ya Ilemela ambao wanaopitiwa huko mtaani na vijana wetu,wasishangae wakiona kazi inaendelea ya kuandika namba na kusajili watoe ushirikiano kwa lolote lile ambalo wanafikiria watahitaji tuwape ufafanuzi sisi kama viongozi wa Wilaya tupo tayari kushirikiana nao kupitia viongozi ambao tumeisha waita na kuwapa maelekezo,”amesema Massala.