Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online
MOJA ya sababu zinazochangia watoto wa kike kukatisha masomo na kuingia kwenye ndoa za utotoni ni pamoja na kutembea umbali mrefu kufuata elimu kunakochangiwa na ukosefu wa mabweni.
Kwa kutambua changamoto hiyo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeamua kuja na mkakati wa ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari zilizopo katika halmashauri hiyo kwa kuanza na shule zilizopo pembezoni kunakofanyika shughuli za uvuvi.
Ambapo mabweni hayo yatasaidia watoto hususani wa kike kuepuka vishawishi wanavyokutana navyo njia wakiifuata elimu ambavyo vimekuwa vikichangia wao kuingia kwenye ndoa za utotoni.
Kwa mujibu wa takwimu za mashirika mbalimbali likiwemo la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF)na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO),umbali wa kwenda shuleni ni moja ya changamoto zinazochangia kukwamisha malengo ya elimu kwa wasichana wengi hususani katika nchi nyingi zinazoendelea.
Pia changamoto ya utoro , mimba na ndoa za utotoni hata mafanikio duni katika masomo na hatimaye maishani kwa wasichana.
Asilimia 73 ya eneo la Wilaya ya Ilemela imezungukwa na maji hivyo shughuli kubwa inayofanyika ni uvuvi na inaelezwa kuwa maeneo zinakofanyika shughuli za uvuvi kuna msukumo mkubwa wa watoto wa kike kuingia katika ndoa za utotoni na kukatisha masomo.
Wanafunzi wa Kisiwa cha Bezi kilichopo Kata ya Kayenze ni miongoni mwa wanaokabiliwa na changamoto ya umbali wa kuifuata elimu.
Kutoka kisiwani Bezi hadi makao makuu ya kata unatumia Kivuko cha Mv.Ilemela kinachotumia takribani saa 1 na dakika 15 hadi 20 na baada ya hapo hadi kufika shule ya Sekondari Kayenze unatumia dakika 20 kwa kutembea kwa miguu.
Hivyo kwa wanafunzi wanaotoka Kisiwa cha Bezi kwa siku wanatumia wastani wa saa tatu(dakika 180) njiani sawa na saa 1: 40 wakati wa kwenda shule na saa 1:40 wakati wakirejea nyumbani.
Nini suluhisho la kuwanusuru watoto wa kike
Suluhisho la kuwanusuru watoto wa kike kutoka Kisiwa cha Bezi kilichopo Kata ya Kayenze, Wilaya ya Ilemela kwa ujumla,ili wasikatishe masomo kwa sababu ya umbali na wasijiingize kwenye ndoa za utotoni ni upatikanaji wa bweni katika shule ya sekondari Kayenze na shule nyingine za sekondari wilayani Ilemela.
Nini jitihada za Ilemela kumkomboa mtoto wa kike.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary, akizungumza kwa njia ya simu na majira mwishoni mwa mwaka 2022,anaelezea mkakati na hatua ambazo wameshachukua ili kupunguza umbali wa kufuata elimu kwa watoto wa kike.
Anaeleza kuwa wanafahamu changamoto ya umbali inayowakabili wananfunzi kutoka Kisiwa cha Bezi kufuata elimu nchi kavu hivyo ujenzi wa bweni utawasaidia kuwaepusha watoto wa kike na changamoto za kukatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ndoa za utotoni.
Nini kipaumbele cha Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Mhandisi Apolinary anaeleza kuwa kipaumbele cha halmashauri kabla ya Juni 30, 2023 wawe wamekamilisha ujenzi wa bweni katika shule za sekondari zilizopo katika Kata za Kayenze, Bugogwa na Sangabuye , hayo ndio maono na malengo.
Kwa mujibu wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014, Serikali itaondoa vikwazo vinavyozuia fursa ya wanafunzi kuendelea na masomo na kukamilisha mzunguko wa elimu katika ngazi husika.
“Kwenye Kata ambazo ni ngumu kimazingira kama Bugogwa, Kayenze na Sangabuye kunakofanyika shughuli za uvuvi na zipo pembezoni, kipaumbele ni kujenga mabweni,” anasema Mhandisi Apolinary na kuongeza;
“Tayari Kata ya Sangabuye tumesha jenga bweni la watoto wa kike na Bugogwa tumepata fedha za Mfuko wa TASAF kiasi cha sh.milioni 80 ili kujenga bweni na hadi sasa ujenzi unaendelea.”
Ambapo ujenzi wa bweni la shule ya sekondari Igogwe Kata ya Bugogwa umefikia zaidi ya asilimia 90 na mwishoni mwa mwezi Aprili bweni litaenda kukamilika hayo yameelezwa na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ilemela.
Mkakati wa kupunguza umbali kwa wanafunzi wa kike Kata ya Kayenze
Mhandisi Apolinary anaeleza kuwa Kayenze ndio kata yao ya mwisho iliyo pembezoni, hivyo mkakati uliopo ni kujenga bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Kayenze ambapo katika bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2022/23 wametenga kiasi cha sh.milioni 100 kwa ajili ya kujenga bweni hilo.
“Mpango wetu umelenga zaidi watoto wa kike hususani wanaotoka Kisiwa cha Bezi wawe na mahali pa kufikia na kulala huku wakiendelea na masomo ili kuwaepusha na umbali unaoweza kuchochea vishawishi ambavyo vitawaingiza katika mimba na ndoa za utotoni,”anaeleza Mhandisi Apolinary.
Hivyo, kwa ujumla mabweni yatasaidia sana watoto wa kike ambao ni wanafunzi wasizurure mtaani na hiyo itawaepusha na vishawishi kutoka kwa watu mbalimbali ikiwemo bodaboda ambao wamekuwa wakiwalaghai.
Wito kwa jamii na viongozi
Mhandisi Apolinary, anaeleza kuwa ni suala la jamii na viongozi kuendelea kuhamasisha wazazi kufahamu umuhimu wa watoto wao kwenda shule kwa ajili ya kupata elimu.
Pia serikali imetoa mwongozo kuwa elimu kuanzia awali hadi kidato cha sita ni bure,hivyo kwa kumkatisha mtoto masomo ili tu aolewe ni kumnyima haki yake ya msingi ya kuendelezwa ambayo inahusu maendeleo ya mtoto kiakili ikijumuisha elimu rasmi na isiyo rasmi, tamaduni,mila na desturi sahihi za jamii yake,kiroho kwa maana ya Imani na vipaji.
Haki hiyo pamoja na nyingine za watoto zinalindwa katika mikataba mikubwa miwili ya haki za watoto , Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto(CRC) wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto(ACRWC) wa mwaka 1990.
Tanzania imeridhia mikataba hiyo miwili inayotoa wajibu kwa serikali,wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na ubaguzi.
“Lazima tuseme ili jamii ielewe maana tusipo sema jamii itaelewa kuwa mila yao ya kuozesha watoto ni kitu cha kawaida,siyo kawaida mtoto anahitimu darasa la saba anatafutiwa mwanaume anaolewa, kwanza anakuwa hajajiandaa na maumbile yake katika umri wake yanakuwa hayajawa tayari kubeba ujauzito, ni changamoto na ni muhimu kuendelea kuongea na wazazi,”anaeleza Mhandisi Apolinary.
Nini mchango wa Mbunge katika kuwezesha mazingira rafiki ya kusoma kwa watoto wa kike.
Akizungumza na Majira/Timesmajira online Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,Kazungu Safari anaeleza kuwa suala la ujenzi wa mabweni ni mkakati wa muda mrefu ambao unaendelea kwa ofisi ya Mbunge kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Serikali Kuu kwenye mashauriano ya kuweka mikakati.
“Tulianza na sekondari ya Sangabuye na tayari tumejenga bweni kwa ajili ya watoto wa kike na tumeendelea na maboresho katika shule ya wasichana ya Bwiru ambapo tumejenga mabweni mapya mawili,”anaeleza Kazungu.
Anaeleza kuwa hayo yote yamefanyika kwa ushirikiano wa halmashauri ambayo imekua ikianzisha msingi Mbunge anatoa saruji kwa ajili ya kufyatua matofali na Serikali Kuu inaletea fedha za kukamilisha ujenzi wa bweni.
“Mpango uliopo kwa shule za sekondari Shibula na Kayenze kwa maana ya kwamba watoto wanaishi japo umbali siyo hoja lakini wanaishi kwenye jamii za wavuvi ambazo mazingira yake siyo rafiki kwa watoto wa kike, kwa hiyo tuna mradi wa hayo mabweni kwenye hizo shule kwa watoto wa kike,”anaeleza Kazungu.
Anasema mbali na shule hizo za kata za pembezoni pia kwa kata za mjini wameanza mkakati wa ujenzi wa mabweni lengo ni kuwaokoa watoto wa kike na changamoto zote zinazochangia ndoa za utotoni na kukatisha masomo.
Katika Kata ya Kawekamo wamejenga mabweni mawili ya watoto wa kike na bweni moja kwa watoto wa kiume ambao watakuwa wanaingia kidato cha nne katika shule ya sekondari Kilimani.
Katibu huyo wa Mbunge anaeleza kuwa ujenzi huo wa bweni umetekelezwa kwa nguvu za Mbunge wa Jimbo la Ilemela kwa kushirikiana na wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo hali ambayo imechochea ufaulu mzuri katika mitihani na shule imekuwa ya mfano katika Wilaya ya Ilemela.
“Tunaendelea kufanya hizo programu za ujenzi wa mabweni katika shule nyingine za sekondari kadri fedha zitakavyo patikana hii yote ni kwa ajili ya kumkomboa mtoto wa kike katika changamoto zinazoweza kukatisha masomo ikiwemo ndoa za utotoni,”anaeleza Kazungu.
Pia anaeleza kuwa sheria za nchi zimetoa maelekezo kuwa mtoto alieko shule aidha wa kike au wa kiume hatakiwi kuoa au kuolewa,kwaio kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Idara ya Elimu wanaendelea kuhakikisha suala la ndoa za utotoni na tabia ya wazazi kuwaozesha kimya kimya watoto wao wanalidhibiti.
“Kweli suala la binti kubeba mimba na familia kumalizana kimya kimya lipo lakini pale tunapolibaini tumekuwa tukichukua hatua,suala la ndoa za utoto na kujihusisha kimapenzi na watoto jamii itambue kuwa ni kosa kisheria na hatutamfumbia macho mtu yoyote na tutaendele kumchukulia hatua kwa mujibu wa sheria,”anaeleza.
Aidha anaeleza kuwa ukimsomesha mtoto wa kike umewezesha jamii nzima akitolea mfano wa Mbunge wa Ilemela ambaye ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Rais Samia.
“Ofisi ya Mbunge kwa kushirikiana na wahisani tunagawa taulo za kike shuleni hii yote ni kuendelea kumuwezesha mtoto wa kike kufikia ndoto zake na asikutane na karaha ya aina yoyote inayoweza kuchangia akakatisha masomo,”.
Nini jitihada za Serikali katika kumkomboa mtoto wa kike.
Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha mtoto wa kike anatimiza ndoto zake za kielimu na hakatishi masomo, katika bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa upande wa elimu ilifuta ada ya kidato cha tano na sita, hivyo kufanya elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi kidato cha sita kutolewa bure bila malipo.
Hatua hiyo itawapa fursa watoto wa kike kuepuka ndoa za utotoni hasa zinazotokana na kisingizio cha mzazi kutokuwa na uwezo wa kumsomesha zaidi.
Aidha Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda katika hotuba yake Mei mwaka 2022, akiwasilisha Bungeni Makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2022/2023 alieleza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini katika sekta ya elimu.
Prof.Mkenda anaeleza kuwa mafanikio ya kuimarisha mazingira hayo ni pamoja na kutoa vibali vya kuanzisha huduma ya bweni katika shule 68 ikiwemo shule za awali na msingi 46 pamoja na sekondari 22,zilizokidhi vigezo kati ya 75 zilizoomba ili kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Anaeleza kuwa serikali pia imewezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa 3,283, mabweni 112 na matundu ya vyoo 8,096.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika