Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Wagonjwa wa kipindupindu wameendelea kuongezeka hadi kufikia zaidi ya 30 mkoani Mwanza ambapo kwa Jiji la Mwanza mlipuko wa ugonjwa huo kwa mara ya kwanza ulitokea Januari 4,2024 ambapo walibainika wagonjwa wawili.
Akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Afya Msingi ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla kilichofanyika Januari 10,2024 ameeleza kuwa kabla ya taarifa mpya, hadi jana usiku Januari 9, mwaka huu, Mkoa ulikuwa na jumla wagonjwa 28 wa kipindupindu.
Ambapo kupitia kikao hicho ametoa maagizo mbalimbali ambayo yatasaidia kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo ikiwemo kuwataka watendaji wa idara za afya kuweka mikakati ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutoa huduma thabiti za matibabu kwa wagonjwa waliopo kwenye vituo vya tiba.
Pia kuhakikisha elimu ya unawaji mikono kwa maji tiririka kwenye maeneo yenye mikusanyiko ipewe kipaumbele huku kila kaya ina kuwa na choo na ihakikishe inakunywa maji safi na salama na kula chakula cha moto.
Aidha ameagiza kusimamiwa kwa maeneo yote ya vilabu vya pombe za kienyeji ili visiwe chanzo cha maambukizi ya ugonjwa huo huku suala la usafi wa mazingira kuanzia sokoni na sehemu zingine yapewe kipaumbele.
Sanjari na hayo amezitaka mamlaka za maji ikiwemo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA),kuhakikisha maji wanayopeleka kwa wananchi yawe yametibiwa vizuri,safi na salama.
Huku Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(TARURA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuzibua mitalo kwani inapoziba uchagu unatuama ambao unasababisha kuzaliana kwa vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa ameeleza kuwa Wilaya zilizoathirika zaidi ni Wilaya ya Magu ambayo ina wagonjwa 21, Ilemela 13.
Amesema toka ugonjwa huo uingie mkoani Mwanza tayari wagonjwa wawili katika Jiji la Mwanza wameruhisiwa baada ya afya zao kuimarika.
Akizungumzia dalili za ugonjwa huo, Dkt. Rutachunzibwa ametaja miongoni mwa dalili zinazojitokeza ni pamoja na kutapika na kuhara kama dalili kuu zingine ni misuli kulegea, na macho kuingia ndani ambapo mgonjwa ataanza kupata dalili hizo kwenye siku ya 1-3 toka ameze kimelea cha ugonjwa wa kipindupindu.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Danstan Ngenzi ambaye ni Ofisa ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa amesema pamoja na mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo, jamii na makundi mengine ikiwemo ya usafirishaji na waganga wa tiba asili yanatakiwa kuzingatiwa katika kuhakikisha wanapatiwa elimu ya kujikinga na ugonjwa kwa kuwa makundi hayo yanakutana na watu wengi.
More Stories
Wajawazito 140, wapatiwa vifaa vya kujifungulia
Wasanii wazidi kumiminika JKCI ofa ya Rais Dkt. Samia
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo