September 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali Kaliua yapokea vifaa vya kujifungulia

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Mawasiliano ya Yas Tanzania, imekabidhi vifaa vya kujifungulia na vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, ikiwa ni mwendelezo wa Kampeni ya Tumaini inayolenga kusaidia huduma za afya ya mama na mtoto.

Msaada huo unatarajiwa kuwapunguzia gharama wajawazito wanaofika kujifungua katika hospitali hiyo, hususan wenye kipato cha chini, pamoja na kusaidia hospitali kukabiliana na mahitaji ya huduma za uzazi.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na maternity kits, vitanda vya uchunguzi kwa wajawazito, kiti mwendo, mashuka, delivery trays na khanga.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Yas Kanda ya Tanganyika Kati, Kamara Kalembo amesema msaada huo ni sehemu ya mwendelezo wa Kampeni ya Tumaini iliyoanzishwa na wafanyakazi wa Yas kwa lengo la kugusa maisha ya jamii wanayoihudumia.

“Tunajivunia kuwa mtandao wa viwango, lakini tunaamini viwango havipaswi kuishia kwenye huduma za mawasiliano pekee. Vinapaswa pia kuonekana katika namna tunavyowajibika kwa jamii,” amesema Kalembo.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kaliua, Dkt. Dismas Bulunja amesema mahitaji ya huduma za uzazi katika hospitali hiyo ni makubwa, huku zaidi ya akina mama 2,650 wakijifungua hospitalini hapo kati ya Januari na Septemba mwaka huu.

Amesema, msaada huo utasaidia kupunguza baadhi ya changamoto za vifaa na kuboresha huduma kwa wajawazito wanaofika hospitalini hapo.

Baadhi ya wajawazito waliopokea msaada huo, Tegemea Awadhi, Amrat Dimanga na Asha Haruna, wakazi wa Kaliua wamesema vifaa hivyo vimewapunguzia gharama za maandalizi ya kujifungua, hasa kwa familia zenye kipato cha chini.

Hospitali ya Wilaya ya Kaliua ni kituo cha tatu kunufaika na Kampeni ya Tumaini, ambayo Yas imeeleza kuwa itaendelea kufikishwa katika maeneo mengine nchini.