January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Homera:Maonesho ya Nanenane kuwa na sura ya Kimataifa

Na Esther Macha, Timesmajira, Online,Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ametangaza kuwa maonesho ya wakulima (nane-nane) mwaka huu yatakuwa na sura ya kimataifa, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa kwenye kilele cha maonesho hayo mwaka uliopita.

Wakati akihitimisha maonesho ya nane-nane mwaka 2022 Rais Samia aliagiza kuwa maonesho hayo yawe ya kimataifa badala ya kitaifa ili kuwa na tija kwa wakulima akisisitiza umuhimu wa kuwaalika wadau kutoka nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 28,2023 Homera amewataka wananchi na wadau wa biashara na uwekezaji kutumia fursa hiyo adhimu kujitangaza kupitia bidhaa zao wanazozalisha ili kupata tija.

Aidha zaidi ya mataifa 30 yamethibitisha kushiriki maonesho hayo ya kilimo, akisisitiza kuwa maandalizi yanakwenda vizuri kwa ushirikiano kati ya ofisi ya Mkoa, wakuu wa mikoa ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo.

‘’Awali nchi 11 zilitarajia kushiriki lakini kutokana na aina ya maandalizi na umuhimu wa maonesho kumekuwa na ongezeko linalopelekea nchi 30 kushiriki, na yatakuwa na kauli mbiu inayosema ‘vijana na wanawake ni msingi imara wa mfumo endelevu wa chakula’’ amesema.

Amesema maonesho hayo yatazinduliwa Julai 25, 2023 na Makamu wa Rias Dkt.Philipo Mpango na kuhitimishwa agosti 8, na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Juma Amos Mkazi Igawilo jijini Mbeya amesema kuwa ujio wa maonesho hayo ya Nanenane kimataifa utaleta fursa za kiuchumi kwa wajasilimali wa ndani na nje katika kuboresha uchumi wao.