November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri Tabora kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji

Na Vincent Tiganya,TimesMajira online,Tabora

SERIKALI imezitaka Halmashauri zilizopo mkoani Tabora kupima maeneo na kuweka miundombinu itakayowawezesha kuyakodisha kwa wafugaji kwa gharama ya sh. 3,500 kwa ekari moja kwa mwaka kwa ajili ya malisho ya mifugo yao na huduma nyingine.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Mashimba Ndaki akitoa jana salamu za wizara yake wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa uwekezaji wa Mkoa wa Tabora

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha Mwongozo wa uwekezaji cha Mkoa wa Tabora.

Amesema maeneo hayo yanatakiwa kuwa miundombinu ya majosho , malambo na huduma nyingine zinazotaji katika mifugo.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akitoa jana salamu za Mkoa wakati wa uzinduzi wa Mwongo wa Uwekezaji.

Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi amesema hatua itasaidia Halmashauri kuongeza mapato yao ya ndani badala ya kukimbizana na mama lishe na Machinga.

Ndaki amesema Mkoa wa Tabora unazo ng’ombe nyingi na Halmashauri zake zina maeneo makubwa ambapo yapingiliwa vizuri yatawasaidia kuepusha migogoro baina ya wafugaji na wakulima.

Ameongeza kuwa maeneo hayo yanaweza kutumika katika uboreshaji wa mifugo kwa ajili ya kuongeza tija ya uzalishaji wa nyama na maziwa.

Ndaki amesema ili Mwekezaji aweze kuweka Kiwanda cha Mazao ya mifugo ni lazima ajiridhishe upatikanaji wa bidhaa ya kutosha mwaka mzima.

Amesema suala la uboreshaji wa mifugo ni jambo la msingi kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji katika sekta hiyo.