May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gomes atema cheche, atamba hakuna kinachoshindikana

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

KOCHA mkuu wa klabu ya Simba Didier Gomes Da Rosa ameendelea kusisitiza kuwa wapinzani wao Kaizer Chiefs wasitarajie kukutana na aina ya mchezo waliouonesha katika mchezo wa kwanza wa robo fainali wa Ligi Mabingwa Afrika ambao walikubali kipigo cha goli 4-0.

Matokeo hayo waliyoyapata Simba yanawapa mlima mrefu wa kupanda kwani ili kufanikiwa kusonga mbele katika hatua yar obo fainali basi wanahitaji kupata ushindi wa goli 5-0 katika mchezo wao wa marudiano utakaochezwa kesho Mei 22 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mchezo huo utaamuliwa na waamuzi kutoka nchini Burundi ambapo ni Pacifique Ndabihawenimana akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Emery Niyongabo, mwamuzi msaidizi namba mbili ni Pascal Ndimunzigo, George Gatogato atakuwa mwamuzi wa akiba huku kamisaa wa mchezo huo ni Mike Letti kutoka Uganda.

Mtathmini waamuzi ni Ali Mohamed Ahmed kutoka Somalia, msimaizi wa mchezo ni Nasiru Sarkintudu Jibril wa Nigeria, Violes Michael Lupondo wa Tanzaia atasimamia mambo ya Covid 19, na wenguine ni Alan Khakame na Ahmed Hussein.

Katika mchezo huo wa awali, licha ya kuongoza kwa umiliki wa mpira kwa asilimia 66 dhidi ya 34 za wenyeji wao Simba haikufanikiwa kupiga shuti lolote lililolenga lango zaidi ya sita ambayo yalikwenda nje dhidi ya mashiti 13 wa Kaizer Chiefs ambao walipiga mashuti 13 na sita yalilenga lango.

Pia Simba walifanikiwa mashuti 597 dhidi ya 303 na Kaizer ambao walipiga pasi sahihi kwa asilimia 74 dhidi ya asilimia 82 za Simba ambao walipiga kona tatu dhidi ya nne za Kaizer.

Kuelekea katika mchezo huo muhimu zaidi za kwa klabu ya Simba lakini na kwa kocha huyo ambaye tayari ameshatimiza ahadi yake ya kuifikisha Simba robo fainali, Gomes amesema kuwa baada ya kubaini na kufanyia kazi makosa mengi waliyoyaona kwenye mchezo wa kwanza, safari hii wapinzani wao watarajie kukutana na kitu tofauti ambacho huenda kikawafanya wasiamini.

Amesema, mambo makubwa waliyoyafanyia kazi kuelekea katika mchezo huo kwanza kushughulikia safu yao ya ulinzi ambayo iliruhusu goli tatu za kichwa na ndio maana wamebadili baadhi ya mbinu ambazo wanaamini zitaweza kuwapa matokeo bora.

Kama kocha anaamini hakuna jambo lisilowezekana na kinachowapa nguvu wachezaji na benchi la ufundi ni imani kubwa ya wanachama, wapenzi na mashabiki wa klabu yao ambao wanaamini wana uwezo wa kupata matokeo bora yatakayowapeleka katika hatua ya nusu fainali.

“Ili kufanikisha hili basi ni lazima tupambane kwa moyo mmoja kama wanaume, sijui nini kitatokea lakini ninaamini kila kitu kinawezekana na kila mmoja atasimamia vizuri majukumu yake ili kuhakikisha timu yetu inafanikiwa kusonga mbele,” amesema Gomes.

Nahodha wa timu hiyo John Bocco amesema, licha ya kutambumu ugumu ulio mbele yao baada ya kupoteza mchezo wa kwanza lakini kila mchezaji ana morali ya hali ya juu kwani wanachotaka kukiona ni timu yao inafuvu kucheza nusu fainali.

Kilicho vichwani kwao kwa sasa ni namna gani wataweza kupindua matokeo hayo na ndio maana wamejaribu kujipa moyo kuwa hakina linaloshindikana kwani kama wenzao walipata matokeo katika uwanja wao wa nyumbani basi ni lazima nao washinde nyumbani kwao.

“Tutaingia uwanjani tukijua tulifungwa ili kufanya dakika 90 za hapa nyumbani kutunufaisha, kwa sasa tunasikiliza kila tunachoelekezwa na viongozi wa benchi letu la ufundi na kurekebisha makosa yet una tuna imani tutapata ushindi na matokeo ambayo yatatufanya kusonga mbele, hivyo tunawaahidi mashabiki kuwa tunakwenda kupambana ili kupata matokeo,” amesema Bocco.