April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Global Education Link yapewa kongole na Serikali

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

SERIKALI imepongeza kazi zinazofanywa na wakala wa elimu nje ya nchi, Global Education Link (GEL) katika sekta ya elimu nchini kwa kuwaunganisha wanafunzi wa Tanzania na vyuo vikuu nje ya nchi.

Pongezi hizo zilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Zena Said wakati alipotembelea mabanda ya kampuni hiyo kwenye maonesho ya vyuo vikuu yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Kwenye maonesho hayo yanayoshirikisha vyuo vikuu mbalimbali nchini, kampuni ya GEL imefanikiwa kuleta vyuo vikuu 10 ambavyo ni washirika wake nje ya nchi kwaaajili ya kuja kuelezea fani wanazotoa.

Wawakilishi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini India na Ukraine wanaohudhuria kwenye maonyesho ya vyuo vikuu kwa mwamvuli wa Global Education Link (GEL), wakizungumza kwenye maonyesho yanayoendelea kwenye viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam

Vyuo hivyo ni Chandigarh, Lovely Professional University (LPU), CT, Maharish Makandeshwar, Pandeet Deendayal Energy, Sharda, Rayat Bahra vya India na VN Karazan na Sum State vya Ukraine.

Katibu Mkuu Kiongozi alisema ni kweli kutokana na uhaba wa fani mbalimbali wanafunzi wa hapa nchini wanalazimika kwenda nje ya nchi kusoma elimu ya juu hivyo kuwa na kiunganishi kama GEL ni jambo la msingi katika kurahisisha upatikanaji wa vyuo hivyo.

“Ni kweli vyuo vyetu haviwezi kuchukua wanafunzi wote sasa nawapongeza nyinyi kwa kazi hii ya kuwaunganisha wanafunzi wetu na vyuo vya nje na pia kwa wale ambao wako tayari kushirikina nasisi nawashukuru sana,” alisema Katibu Mkuu Kiongozi.

Awali, Mkurugenzi wa GEL, Abdulmalick Mollel alimweleza kuwa kampuni yake imekuwa ikishirikiana na vyuo hivyo kuwapeleka wanafunzi wa Tanzania kwa kozi mbalimbali ikiwemo mpango wa kubadilishana awanafunzi, exchange program

Mollel alisema wakati nchi mbalimbali duniani zina kozi nyingi sana za afya kwa Tanzania bado hazijawa za kutosha hivyo wanafunzi wanaotaka kozi hizo wamekuwa wakiwaunganisha kwenda kusoma kwenye nchi hizo.

“Tumezungumza na vyuo vingi vya nje ya nchi kwamba sisi tuna wanafunzi wengi na wamekubali kuwachukua wanafunzi hao kwa gharama za hapa hapa ndani wakati sisi tunajipanga kuongeza kozi za afya hapa nchini,” alisema Mollel.

Wananchi mbalimbali wakiendelea kupata maelelezo kutoka kwa maofisa wa wakala mkubwa wa kuunganisha wanafunzi na vyuo vikuu nje ya nchi, Global Education Link kwenye maonyesho ya vyuo vikuu yanayoendelea jijini Dar es Salam.

Alisema baadhi ya vyuo vimeahidi kufungua matawi hapa nchini baada ya kuona mahitaji makubwa ya kozi wanazofundisha ambazo wanafunzi wa Tanzania wamekuwa wakizifuata kwenye mataifa yao.

Alisema pia baadhi ya vyuo hivyo vya nje vitaingia makubaliano na vyuo vya hapa nchini kuhusu namna ya kufanyakazi pamoja katika utoaji wa elimu ya juu.

Mollel alisema ujio wa vyuo hivyo ni fursa kwa vyuo vya Tanzania kuangalia namna ya kushirikiana kwenye kozi mbalimbali ikiwemo kubadilishana wanafunzi wanaoendelea na masomo ili kupeana uzoefu.

Wanafunzi na wazazi wakiendelea kupata maelelezo kutoka kwa maofisa wa wakala mkubwa wa kuunganisha wanafunzi na vyuo vikuu nje ya nchi, Global Education Link kwenye maonyesho ya vyuo vikuu yanayoendelea jijini Dar es Salam

“Mfano mwanafunzi anaweza kusoma miaka miwili India akaja kumalizia hapa Tanzania na wahapa anaweza kusoma mwaka akamalizia kwenye chuo cha nje, haya ni mambo ambayo vyuo vinapaswa kuangalia namna ya kushirikiana,” alisema Mollel.