Na Penina Malundo, TimesMajira Online
TANGU kutengenezwa kwa gari ya kwanza mwanzoni mwa miaka ya 1900, marekebisho kadhaa yamekuwa yakifanyika kwa ajili ya kuimarisha usalama wa dereva na abiria kwenye magari.
Asilimia kubwa ya vifaa vingi vya kinga vilikuwa vikiwazingatia zaidi usalama wa watu wazima bila kujali usalama watoto wanapokuwa ndani ya magari.
Kuanzia mwaka 1930, vilianza kutengenezwa viti maalumu kwa ajili ya kuwakinga watoto pindi ajali inapotokea ndani ya gari.
Vizuizi vya watoto kwenye magari ni viti maalumu vinavyounganishwa kwenye viti vya magari,lengo ikiwa ni kuwakinga watoto mara ajali inapotokea.
Asilimia kubwa ya vizuizi hivi vina uwezo wa kubeba watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi 12 na uzito ukiwa tofauti.
Mara nyingi vizuizi hivyo vya watoto wachanga uwekwa kwenye viti vya nyuma vya magari binafsi ambapo usaidia kupunguza madhara inapotokea ajali au mtikisiko wa ajali.
Licha ya kuwepo kwa umuhimu wa vizuizi hivyo, Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 nchini Tanzania, haijaweka wazi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kumlinda mtoto dhidi ya hatari yoyote inayoweza kutokea ndani ya gari.
Mbaya zaidi katika Sheria hii ya Usalama Barabarani (1973), kifungu cha 39(4)(b) kinatambua watoto wawili, wenye umri unaozidi miaka 3 na usiozidi miaka 12 kama abiria mmoja wanapopanda katika mabasi hali inayowafanya watoto hawa kukosa usalama pindi ajali inapotokea au dereva akifunga breki gafla.
Mnamo Mei, 2011 katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ilitangazwa muongo wa hatua za usalama barabarani 2011- 2020 ili kukabiliana na ongezeko la kasi kwa majeraha yanayohusiana na ajali za barabara na vifo vinavyotokea ulimwenguni kote.
Baraza lilitoa mapendekezo ya kuendelea kusisitiza usalama wa barabarani katika mpango wa maendeleo endelevu hadi ifikapo mwaka 2030 katika lengo namba nne la kuhakikisha usalama wa barabarani unatekelezwa na mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji uliopangwa katika Mpango wa maendeleo endelevu.
Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi nchini kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani zinaonyesha uhalisia na uhitaji kuwa na vizuizi vya watoto kulinda maisha yao.
Kwa mwaka 2017, watoto wa umri kati ya miaka saba hadi 12 jumla ya watoto 60 walifariki dunia na waliojeruhi wakiwa 230 ,huku kwa mtoto wa mwaka mmoja hadi miaka saba takwimu inaonyesha kuwa jumla ya watoto 11 walifariki dunia na waliojeruhiwa wakiwa 143 huku watoto wenye umri kati ya miaka 13 hadi 18 waliofariki walikuwa watoto 223,hii imefanya kuwe na jumla ya watoto 294 waliofariki na waliojeruhiwa ni takribani watoto 832 kwa mwaka huo.
Aidha katika kipindi cha mwaka 2018 watoto wadogo kati ya umri wa mwaka mmoja hadi saba jumla ya watoto wanne walikufa huku kwa umri wa miaka saba hadi 12 waliokufa walikuwa watatu na watoto kati ya umri wa miaka 13 hadi 18 takribani watoto 73 na kufanya jumla ya watoto 94 kufariki na waliojeruhi kuwa 258.
Kwa mwaka 2019, takwimu inaonyesha inaonyesha watoto wa umri kati ya mwaka mmoja hadi saba hakukuwepo na kifo,watoto kati ya umri wa miaka Saba hadi 12 walifariki watoto 10 huku watoto kati ya umri wa miaka 13 hadi 18 takribani watoto 42 walifariki dunia na kufanya jumla ya watoto waliofariki kwa mwaka huo kuwa 52 na kujeruhiwa watoto 177.
Kutokana na kushuka kwa idadi ya vifo kwa upande wa watoto ni kutokana na utoaji wa elimu kwa watumiaji wa vyombo vya moto wakiwemo madereva kwani kundi la watoto wadogo ni kundi linalohitaji usimamizi.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Dunian (WHO) matumizi ya vizuizi maalumu vya watoto (child restraints) ni njia pekee inayoweza kuwaokoa watoto dhidi ya madhara yatokanayo na ajali.
Gharama ya ununuaji wa vizuizi hivyo vya watoto vimetaja ni moja ya Changamoto ya wamiliki wengi wa magari kushindwa kumudu kununua viti hivyo.
Ukubwa wa gharama wa viti hivyo vinachangia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara wa vifaa hivyo kuongeza bei kuwa juu kutokana na bidhaa hiyo kutokuwa nyingi katika baadhi ya maeneo.
Akizungumza hivi karibuni, Wakili Rehema Mmanga amesema Sheria ya Usalama wa Barabarani haijaweka ulinzi wowote wa mtoto akiwa katika gari kwa kutumia kizuizi.
Anasema kwa mujibu wa sheria hiyo inatambua kuwa sio lazma kutumia kizuizi cha mtoto kwani sheria hiyo ipo kimya na haiongei chochote juu ya ulinzi wa mtoto ndani ya gari.
‘’Suala la vizuizi vya mtoto halijazungumzwa katika sheria ya barabarani iliyopo labda iingie katika marekebisho yaliyopendekezwa kwa wadau mbalimbali wa masuala ya usalama barabarani,”amesema na kuongeza
“Kutokuwa na sheria hii inaonyesha wazi wazazi au walezi kutozingatia kutumia vizuizi hivyo katika kuwasaidia watoto kuweka ulinzi wao wanapokuwa ndani ya magari,” amesema
Aidha Wakili Mmanga anasema kutokana na sheria ya mwaka 1973 kutosema suala lolote kuhusu vizuizi hivyo inachangia kutokuwa na uelewa kwa wananchi kutotambua umuhimu wa vizuizi hivyo.
Amesema amefanya utafiti mfupi kwa watu juu ya ufahamu wao kuhusu vizuizi hivyo wameonekana kutojua suala la vizuizi vya watoto kutokana na kutokuwa na uelewa.
“Nimepata nafasi ya kuuliza watu wachache juu ya kujua umuhimu wa vizuizi vya watoto na imeonyesha kuwa hawajui chochote na kufanya gharama ya uuzaji wa kifaa hicho kuwa juu,’’ amesma
Wakili Mmanga amesema kutokana na bidhaa za vizuizi kuwa vichache madukani na kufanya bei yake kuwa juu.
“Sheria ikifanyiwa marekebisho na kutamka wazi umuhimu wa vizuizi ni lazma alafu pia jamii ielewe kuwa ni lazma kuwa kizuizi ndani ya gari na sheria itamke kuwa edapo mtu akikamatwa kwa kosa la kutokuwa na kizuizi cha mtoto apewe adhabu au faini,’’ amesema
Akizungumza Vizuizi hivyo. Amesema bidhaa hii ya vizuizi vya watoto ni adimu watu wengi hawajui kwani kiti kimoja cha mtoto ni kiasi cha sh 150,000 ikilinganishwa na uzito wa mtoto.
Akizungumzia, gharama za viti hivyo, mmoja wa wauzaji wa vizuizi hivyo kariakoo jijini Dar es Salaam ,Said Jumaa amesema vizuizi hivyo uuza kati ya kiasi cha sh. 150,000 hadi Sh 200,000 kwa kiti moja.
Amesema na viti hivi uuzwa kulingana na umbo la mtoto pamoja na kilo zake kutokana na kutofautiana.
“Siti hizi, kwa kuwa haziji na magari, watumiaji wa magari hulazimika
kuja kuzinunua kwa ajili ya ulinzi wa watoto wao wanapokuwa wamewapakia ndani ya magari yao,’’ amesema
Akielezea Changamoto ya uuzaji wa vizuizi hivyo anasema Changamoto ni kubwa kutokana na wao uingiza viti vichache kwa sababu ya kasi ya ununuaji ipo chini.
Pia amesema mara nyingi siti hizo uchukua muda mrefu kununuliwa, ambapo inaweza kukaa dukani hata miezi kadhaa .
Beatrice Methew mmoja wa wamiliki wa gari ndogo aina ya mark 11,anasema anasema suala la gharama kubwa ya vizuizi limekuwa likiwakatisha tama watu wengi kutokana na hali ya uchumi, manunuzi ya vizuizi hivyo kuwa ya gharama kubwa .
“kwa hali ya sasa ilivyo kwa matumizi ya kila kizuizi ni miaka miwili hadi mitatu na kinauzwa si chini ya 150,000,” amesema
Naye Ofisa Programu Masuala ya Usalama Barabarani kutoka Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Mercy Kessy amesema sheria ya sasa ya usalama barabarani ya mwaka 1973 haiongelei kabisa masuala ya viti vya watoto ikiwa na maana kwamba hakuna kifungu chochote kinachoongelea utumiaji wa viti vya watoto kwenye Magari.
Amesema kutokana na sheria ya sasa ipo kimya,wadau wa masuala ya usalama barabarani ikiwemo TLS, wameweza kutoa mapendekezo yao ya kuwepo kwa mabadiliko ya sheria ya usalama wa barabarani kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani na vifo vitokanavyo na ajali.
Messi amesema mojawapo ya mapendekezo waliyoyatoa ni pamoja na kuwepo na viti vya watoto katika magari binafsi pamoja na magari ya abiria ili kuokoa maisha ya watoto pindi ajali inapotokea .
“Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watoto wanapokaa katika viti maalum kwenye magari yaani ‘ Child Restraints’ kwa kuzingatia uzito na umri inapunguza kwa kiasi kikubwa ongezeko la vifo vya ajali kwa watoto,” amesema.
Amesema kupitia mapendekezo ya wadau baada ya kufanya tafiti kwa nchi nyingine ni kuwa sheria ya sasa inayoenda kufanyiwa marekebisho iweke kifungu hicho cha kuweka ulazima wa magari binafsi na magari ya wa abiri yaani (Public Transport) kuweka vizuizi vya watoto katika magari yao.
Amesema kwa tafiti zilizofanywa na Global Road Safety Partnership:Seat Belts Facts Sheets, 2015 inaonyesha nchi zinazotumia vizuizi vya watoto inapunguza madhara ya kupata ajali takribani asilimia 70.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani