April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Familia ya Lowassa: Asingekuwa Rais Samia baba asingefika hata hiyo juzi

Na Mwandishi wetu,Timesmajira Online,Dar

FAMILIA ya Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Lowassa, imesema baba yao aliugua kwa muda mrefu na kama asingekuwa Rais Samia Suluhu Hassan, asingefika hata hiyo juzi (Februali 10) siku aliyofariki.

Hayo yamesemwa na mtoto wa Lowassa, Fredrick Lowassa kwa niaba ya familia wakati wa kuaga mwili Lowassa kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, leo.

Fredrick ambaye pia ni Mbunge wa Monduli amesema familia imepokea kifo cha baba yao kwa moyo wa amani kwa sababu aliugua kwa muda mrefu.

“Kama waliovyosema mashuhuda hapa, kwa kweli baba alipambana hadi dakika ya mwisho, lakini kwa yaliyotokea yote ni kazi Mungu, tunasema muache baba akapumzike.” Amesema Frederick.

Amesema familia inatoa shukurani za familia kwa Rais Samia. “Niseme ukweli kama asingekuwa Rais Samia, baba yetu asingefika hata hiyo juzi, Mama Samia katika familia yetu amekuwa ni ndugu, amekuwa mama mzazi, amekuwa ni mlezi wetu, kwa kweli hatuna cha kumlipa.”

Amesema siku Rais Samia anaondoka kuelekea Italia asubuhi, tayari hali ya baba yao ilikuwa imebadilika, lakini alimtuma Mkuu wa Majeshi (Jenerali Jacob Mkunda) alikwenda hospitali akawa anampa taarifa kila baada ya nusu saa hadi alipokutwa na mauti saa 8 mchana.

“Tulikuwa na mkuu wa majeshi kupigania maisha ya baba , tunamshukuru sana Mama Samia Suluhu Hassa,” alisema Frederick na kuongeza kwamba msimba huo sio wa ukoo wa Lowassa, kwani wote ni mashuhuda jinsi baba yao yalivyokuwa mlezi na mzazi wa watu wengi.

Wazazi na watoto ambao wanasoma shule za kata leo wanaomboleza , watoto na wazazi ambao wanakunywa maji kutoka Ziwa Victoria leo wanaomboleza, watoto na wazazi ambao wanasomesha watoto pale UDOM leo wanaomboleza, tunashukuru Mungu kwa zawadi ya maisha yake.” Alimaza Fredrick.

Akitoa salamu za mahakama, Jaji Mwambegele amesema uvumilivu aliokuwa nao Lowassa ni funzo kubwa kwa Mahakama na wataendelea kuishi mtazamo huo.

“Mahakama ya Tanzania inaungana na Watanzania wote kuomboleza msiba huu mzito.

Mahakama inamfahamu marehemu Lowassa kama mwanasiasa mwenye moyo wa uvumilivu. “Ni mwanasiasa ambaye alikuwa na ngozi ngumu ya kisiasa, sisi watu wa mahakama tulimuona Lowassa akiuishi usemi ‘silence is golden’ hili tunalichukua kama funzo,”amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Anamringi Macha alisema kila mtu kwa nafasi yake ana la kujifunza kutoka kwa Lowassa, hivyo ni muhimu kuyachukua mazuri yake na kuliendeleza taifa.

“Yote yaliyosemwa ni mengi na tumeyasikia, tunaomba kila mmoja wetu kwa nafasi yake aone ni kipi anaweza kukichukua na kulijenga Taifa. “Sehemu kubwa ya maisha ya Lowassa yalikuwa CCM, hivyo tuna vingi ambavyo tumejifunza kutoka kwake,” amesema Macha.