April 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Falsafa ya Kazi na Utu inavyotafsiriwa kwa vitendo na MSD

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOline, Dodoma

“KAZI na Utu, Tunasonga Mbele.” Hiyo ni falsafa inayotumiwa na Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa imebeba maana pana na yenye ujumbe mzito.

Lakini Watanzania wakiona kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika sekta ya afya kupitia Bohari ya Dawa (MSD) watajua maana halisi ya falsafa hiyo.

Leo ni Watanzania wachache wanaoweza kuwaza kuwa afyà bora waliyonayo inayowawezesha kufanya shughuli zao za kila siku nyuma yao kuna MSD.

Ili Mtanzania aweze kujua hilo ni hadi apate changamoto na kuhitaji kwenda hospitali kupata huduma za afyà.

Wale wanaofika hospitali kupata kupitia vifaa tiba vya kisasa na uwepo dawa za uhakika watakuwa mashuhuda wa jinsi MSD inavyotekeleza kwa vitengo maono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania wanapata huduma bora za afya kuanzia watoto njiti hadi wazee.

Hiyo inaonesha jinsi Serikali ya Rais Dkt. Samia inavyojali afya za Watanzania .

Lakini wataelewa kuwa Rais Dkt. Samia , anapigania afya za Watanzania, bila kujali wale wanaokesha mitandaoni wakisema Serikali haijafanya kitu, lakini wakienda hospitali wanapata huduma kupitia vifaa tiba vya kisasa kutoka MSD.

Wale waliokulia vijijini kama mimi wanasahau kuwa zamani wananchi walipokuwa wakiona gari la MSD wanashangilia wanajua wamepelekewa dawa, lakini sasa wamezoea kuyaona,kwani magari hayo wanayaona mara sita kwa mwaka yakiwapelekea dawa na vifaa tiba vya kisasa, hawashangilii tena maana dawa zipo muda Wote.

Wiki iliyopita nilikuwa miongoni mwa wanahabari walioshuhudia kazi kubwa inayofanywa na Serikali kupitia MSD kwa kufanya uwekezaji mkubwa sekta ya afyà.

Kazi kubwa inayofanywa na MSD inaweza kushuhudiwa na wanahabari waliotembelea hospitali zinazohudumiwa na MSD Kanda ya Kati Dodoma.

Mafanikio hayo mbele yake ipo MSD ambayo imepewa majukumu ua uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya.

Kwa sasa MSD inasambaza wastani wa asilimia 81 hadi 83 ya bidhaa za afya katika vituo vya umma, huku kiasi kilichosalia kikitolewa na wadau wengine katika ngazi za mikoa.

Mkurugenzi Mkuu MSD, Mavere Tukai amesema sekta ya afya ni mhimili mkuu wa usalama wa taifa, akisisitiza kuwa ustawi wa afya ya jamii una uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Tukai ameyasema hayo katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika katika Ofisi za MSD Kanda ya Kati jijini Dodoma

Ameabainisha kuwa,jamii isiyo na afya njema haiwezi kuwa salama wala kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.

“Afya ni usalama wa taifa. Jamii ikiwa haina afya haiwezi kuwa salama, na bila usalama hakuna uzalishaji, hivyo hakuna uchumi,” amesema.

Amefafanua kuwa,sekta ya afya inaweza kufananishwa na stuli ya miguu mitatu inayojumuisha fedha, huduma na bidhaa, huku MSD ikiwa na jukumu la kusimamia upatikanaji wa bidhaa za afya.

Ameonya kuwa, endapo mguu mmoja kati ya hiyo utayumba, sekta nzima itakuwa katika hatari ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Tukai amesisitiza kuwa, MSD ina wajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora, salama, zenye gharama nafuu na zinazowafikia wananchi kwa wakati. Amebainisha kuwa, taasisi hiyo ni kiungo muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinakuwa kamilifu nchini.

“Tunasimamia upatikanaji wa uhakika wa bidhaa za afya.

Bila bidhaa hizo, sekta ya afya haiwezi kuwa kamili.Tunahakikisha bidhaa zote ni bora, salama na zinapatikana kwa wakati,” ameeleza.

Tukai amesema kuwa, MSD imepiga hatua kubwa katika kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, ambapo kiwango cha utimilifu kimeongezeka kutoka asilimia 40 katika kipindi cha miaka minne iliyopita hadi zaidi ya asilimia 80 kwa sasa.

Katika hatua nyingine Mganga Mfawindhi wa Hospitali ya Dodoma Dkt. Joshua Mwalongo, ameishukuru MSD kubwa wanayofanya , kwani hata pale wanapoomba dawa kwa dharula wanapelekewa haraka.

Ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma wakati alipozungumza na Wahariri wa vyombo vya Habari walipotembelea hospitali hiyo kuona huduma zinazotolewa kupitia vifaa tiba na dawa kutoka MSD.

Amesema sh.Bilioni 2.7 zimetumika hadi sasa katika ujenzi wa Hospitali ya Jiji la Dodoma, huku MSD ikiipatia vifaa tiba vya zaidi ya Milioni 100/.

Hospitali hiyo ambayo hadi sasa ina majengo 10 ya kutolea huduma , imeanza kutoa huduma Januari mwaka 2025 ambapo kwa sasa inatoa huduma kwa wagonjwa 700 kwa mwezi.

Dtk. Mwalongo ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa ujenzi wa Hospitali hiyo ambayo imepunguza msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na Hospitali ya Makole ambapo wanamchi watapata huduma bora na kisasa karibu na maeneo yao, huku vifaa tiba vinavyotolewa na MSD vikiwa vya kisasa.

Awali Meneja MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa amesema kupatika kwa Hospitali ya Jiji sambamba na vifaa tiba vinavyosambazwa MSD itasaidia kutoka huduma za uhakika na kupunguza msomgamano katika Hospitali zingine .

Amewahakikishia Watanzania kuwa. MSD itaendelea kupeleka Dawa na vifaa tiba vya kisasa kwa wakati.

Katika hatua nyingine MSD imeelezwa hatua mbalimbali za mafanikio ambazo zimefikiwa ba bohari hiyo katika kipindi cha miaka minne.

Mfamasia kutoka kitengo cha Mipango,Ufuatiliaji na Tathimini Lilian Magesa kutoka MSD amesema kuwa kumekuwepo na mafanikio katika kipindi cha miaka minne 2021/22 hadi mwaka 2024/25.

Amefafanua katika kipindi cha miaka minne mapato ya MSD yameongezeka kwa asilimia 103 kutoka Sh.Bilioni 315.12 hadi kufikia kiasi cha Sh.Bilioni 640,5 mwaka 2024/25.

Pia mafanikio mengine ni kuongezeka kwa upatikanaji wa bidhaa za afya ashiri kutoka asilimia 42 mwaka 2021/22
hadi kufika asilimia 73 Machi, 2026.



“Hali ya utimizaji wa mahitaji wa vituo vya kutolea huduma za afya umeendelea kuongezeka kutoka asilimia 4l hadi kufikia asilimia 77 katika kipindi cha miaka minne.”

Pia amesema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa mizunguko ya usambazaji wa bidhaa za afya kwenda vituo vya kutolea
huduma za afya kutoka mizunguko minne kwenda mizunguko sita kwa mwaka huku ununuzi wa bidhaa za kuwezesha uzazi pingamizi ( CEmONO) umefikia asilimia 100 ya
MS.

Magesa ameongeza kuwa mafanikio mengine mashine 162 za kusafisha damu(dialysis) zimesambazwa kutoka mashine 60 mwaka 2021/2022 zilizogharimu S h.bilioni 10.14

Pia kukamilisha ujenzi wa maghala ya kisasa yanayokidhi viwango vya uhifadhi na kuanza kutumika katika Kanda ya Dodoma na Mtwara -mita za mraba 12,000.Aidha kuanza kwa ujenzi wa ghala la Chato mkoani Geita lilifikia asilimia 42 ya utekelezaji.

Mafanikio mengine ni uanzishwaji wa kampuni tanzu ijulikanayo kama MSD Medipharm Manufacturing Company yenye jukumu la kusimamia uzalishaji unaotekelezwa kibiqshara na kwa ufanisi mkubwa .

“Pia kiwanda cha mipira ya mikono -Idofi kukamilika na kuanza kazi rasmi ya uzalishaji Februari 2024 pamoja na ongezeko la thamani ya bidhaa zinazonunuliwa kutoka kwa wazalishaji wa ndani kutoka Sh.bilioni 15.90 zilizonunuliwa mwaka 2021/22 hadi Sh.bilioni 98.72 mwaka 20/2024/25.”

Kuhusu changamoto alisema mojawapo ni uhaba wa mtaji wa kuwezesha;Ununuzi wa bidhaa za Afya toshelevu kwa kiwango cha miezi 5, Ujenzi wa miundombinu toshelezi na inayokidhi viwango vya uhifadhi pamoja na ushiriki na uanzishai wa viwanda vya bidhaa za afya.

Pia uwepo wa madeni, Washitiri kuchelewa kuleta bidhaa za afya kulingana na mikataba,ufinyu wa maeneo ya kuhifadhia bidhaa za afya licha ya kuongezeka kwa idadi ya watu na mahitail na utegemezi wa uagizaji kutoka nje ya nchi kutokana na uwezo hafifu wa viwanda vya ndani.

Naye mwakilishi wa Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Magreth Makilika ameipongeza MSD kwa kuendeleza ushirikiano na vyombo vya habari, akieleza kuwa hatua hiyo ni mfano bora wa uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma.

Kwa upande mwingine, mwakilishi kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Hassan ameeleza kuwa, wanahabari wana jukumu muhimu katika kuunganisha jamii na taasisi za serikali pamoja na kuelimisha umma kuhusu masuala ya maendeleo.

Amesisitiza kuwa, vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kuchochea maendeleo ya jamii kwa kutoa taarifa sahihi, kuibua changamoto na kusaidia katika utoaji wa suluhisho kupitia mijadala ya umma.

Akizungumza kwa niaba ya wahariri, Mhariri Mkuu wa Gazeti la Habari Leo, Mgaya Kingoba ameipongeza MSD kwa kuandaa semina hiyo, akisema kuwa imechangia kuongeza uelewa sahihi kuhusu sekta ya afya na kupunguza upotoshaji wa taarifa.

Amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa sahihi na zenye kuaminika kwa wananchi, hasa kuhusu mafanikio ya uwekezaji wa serikali kupitia Wizara ya Afya na MSD.

“Nafasi yetu ni kuwa daraja kati ya serikali na wananchi kwa kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia walengwa. Hili linahitaji weledi na uwajibikaji wa hali ya juu,” amesema.

Ushirikiano wa MSD na vyombo vya habari ni nyenzo muhimu katika kuboresha huduma za afya .

Mmmmmmmm