Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa chanjo ya UVIKO-19 ni moja ya afua muhimu katika mapambano dhidi ya corona,hivyo Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha wananchi wanapata chanjo hiyo.
Ambapo imekuwa ikitumia viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya vitongoji kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuchanja chanjo hiyo jambo ambalo limeonesha mafanikio baada ya mwitikio wa watu kuongezeka kujitokeza kupata chanjo hiyo tofauti na awali wakati zoezi hilo nchini hapa lilivyo anza.
Akizungumza na timesmajira Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza Amos Kiteleja, ameeleza kuwa katika zoezi la utoaji chanjo ya uviko-19 lilianza Agousti 3,2021 katika vituo 27 na baadae kuongezeka hadi vituo 40
Septemba 21,2021 walizindua mpango shirikishi na harakishi kwa kutoa chanjo ya uviko-19 katika vituo 346 Mkoa mzima sasa wanatoa kwenye vituo 355 ambapo viongozi walishiriki katika mpango huo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliyekuwa anapita maeneo mbalimbali kuhamasisha watu kuchanja huku Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe inaonekana kufanya vizuri katika zoezi hilo ukilinganisha na halmashauri nyingine zilizopo mkoani Mwanza.
Kiteleja ameeleza kuwa,awali watu walikuwa hawataki kuchanja hali iliyochangia zoezi hilo kutokwenda vizuri lakini baada ya kufanya juhudi na mikakati mbalimbali ili kuhakikisha watu wengi wanachanjwa ikiwemo ya utoaji elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa chanjo ya Uviko-19 imesaidia watu kukubali kupata chanjo hiyo.
Ambapo tangu kuanza kwa zoezi hilo mpaka Juni 11,2022 wameweza kuwachanja takribani watu 479,094 angalau kwa dozi ya kwanza huku malengo hadi kufikia Desemba ni kuchanja watu zaidi ya milioni 1.2 sawa na asilimia 70.
“Wakati tunaanza zoezi la utoaji chanjo hali haikuwa nzuri mwitikio ulikuwa mdogo baada ya kutoa elimu idadi ya watu kupata chanjo iliongezeka, tumechanja watu wengi, tunaendelea kuchanja wengine mpaka tuhakikishe wote wamepata chanjo tuwakinge dhidi ya uviko-19 kwani ugonjwa huu umeleta athari kubwa kiuchumi na kwa maisha ya watanzania,” ameeleza Kiteleja na kuongeza kuwa
Pia ameeleza kuwa upotishaji juu ya chanjo ya uviko-19 umebaki kwa watu wachache ambao hawajaelewa umuhimu wa chanjo awali mitandao ya kijamii ilitumika sana katika kupotosha lakini sasa hivi imepungua ndio maana hata kukubalika kwa wananchi kuchanja ni kutokana na jamii kuwa na uelewa huku tangu kuanza kuchanja hakuna mtu aliyepata madhara hivyo waliona ili kuwa upotishaji na kwa sasa watu wanaojitokeza kwa wingi kupata chanjo.
“Walikubali kuchanja sababu waweze kujikinga na madhara ya ugonjwa wa corona,chanjo hazina madhara na walielewa umuhimu wa chanjo,wachache sana mbao hukataa kuchanja ni kwasababu hawajapata elimu ya kutosha wanapo elimishwa hukubali kuchanjwa na
wengi wanaokubali kuchanjwa kwa sasa ni baada ya kuona chanjo hazina madhara na zinawakinga dhidi ya magonjwa,”.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Dkt.Getera Nyangi,ameeleza kuwa Ukerewe ni moja ya halmashauri mkoani Mwanza inavyofanya vizuri katika afua za chanjo ya uviko-19 ambapo takribani miwili iliopita duniani ilikubwa na janga la ugonjwa wa corona ambapo afua pekee ya usalama ni kuhakikisha wananchi wengi wanachanja.
“Ukerewe tunafanya vizuri sababu kwa asilimia 95 zoezi tumeshirikisha jamii,mfano watu wanaoishi karibu na jamii ni viongozi wa kitongoji Wana ushawishi ambao utamfanya mtu akubali hii chanjo,wote tunakubali wakati chanjo hii imeingia kulikuwa na maneno mengi hasi ambapo wengine walikuwa wanasema ukichanjwa utabadilika kuwa jini au utakufa,kumshawishi mwananchi lazima utumie viongozi wenye ushawishi mkubwa kutoka katika jamii na Ukerewe tunawatumia viongozi ngazi ya kitongoji,”ameeleza Dkt.Nyangi.
Dkt.Nyangi ameeleza kuwa zoezi la utoaji chanjo Ukerewe lilianza Agousti 5,2021 na zoezi halikwenda vizuri jambo walilokuja kugundua ni kuwa walitumia nguvu kubwa kuwasubilia wagonjwa kwenye vituo baada ya kugundua hivyo waliamua kuwafuata watu kwenye maeneo yao ngazi ya jamii ikiwemo kwenye magulio.
Pia Ukerewe moja ya shughuli kubwa ni uvuvi na kuna kambi kubwa za uvuvi na walibaini kuwa kati ya kundi kubwa ambalo ni wepesi kukubali chanjo hizo ni wavuvi ambao ukiwapelekea taarifaa na kumuelewesha vizuri uwezekano wa kukataa kuchanja ni asilimia ndogo.
“Mwitikio wa uchanjaji kwa wavuvi Ukerewe ni mkubwa ambao ni moja ya njia iliochangia mafanikio ya utoaji wa chanjo ya uviko-19 kwa Wilaya ya Ukerewe,katika vipindi viwili kuanzia mwezi Agousti hadi Septemba,2021 mwishoni tulikuwa tumechanja watu asilimia 7 tu lakini baada ya kubadilisha mbinu za kufikia wananchi tunaongelea asilimia 66 na kwa sasa hatuna chaguo jingine ni kufikia walengwa wote wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea,”ameeleza Dkt.Nyangi.
Kwa upande wake mmoja wa wavuvi wa mwalo wa Butuja, Emmanuel Nyagwesi,ameeleza kuwa awali wakati zoezi la utoaji chanjo ya uviko-19 limeanza nchini hakuwa tayari kuchanjwa kwa sababu alikuwa hajapata elimu wala uelewa wa chanjo hiyo.
Ila baada ya kuelimishwa juu ya chanjo hiyo na kutambua kuwa ni muhimu katika kujikinga na kupambana na uviko-19 aliamua kuchanja na tangu apate chanjo hiyo hakuna mabadiliko yoyote yenye athari katika mwili wake kama ambavyo watu walivyokuwa wanazungumza.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best