Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga
WITO umetolewa kwa vyama vya siasa nchini hapa kuacha siasa za mihemko na badala yake kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia usajili na uendeshaji wa vyama hivyo ili kulinda amani na utulivu wa taifa.
Kauli hiyo imetolewa jana na aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2025 kupitia chama cha National League for Democracy (NLD) Doyo Hassan Doyo,ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho,wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga, kuhusu mwenendo wa siasa nchini hapa.

Ambapo amesisitiza kuwa hakuna chama, mwanasiasa au mwanaharakati anayepaswa kujiona yupo juu ya sheria huku akiitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kusimamia sheria bila woga wala upendeleo.
Doyo amesema hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukiandikia barua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuomba ufafanuzi kuhusu kauli ya mmoja wa viongozi wake ni ishara kuwa sheria inasimamiwa kwa usawa kwa vyama vyote vya siasa nchini.
Amesema kuna wanaharakati na wanasiasa ambao wanajiona wapo juu ya sheria na wana uwezo wa kusema chochote huku wakitishia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakisahau kuwa ofisi hiyo ipo kisheria na iko imara.
Katika hatua nyingine, Doy ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kile alichodai kuwa ni uthubutu wa kuchukua hatua kwa vyama mbalimbali vya siasa bila upendeleo.
“Msajili aliwatandika barua CHADEMA wakahangaika nayo,licha ya kuwepo kwa malalamiko na mjadala mkubwa wa kisiasa lakini mwisho wa siku chama hicho kilitoa majibu na kupeleka maelezo yao. Hii inaonyesha kuwa sheria lazima ifuatwe,” amesema Doyo na kuongeza:
“Tumeona Msajili amechukua hatua kwa kuiandikia barua CCM ili nao watoe maelezo ya kina kuhusu kauli za viongozi wao. Hii inaongeza matumaini makubwa kwa vyama vya siasa pamoja na wananchi kwa ujumla,”.
“Tuna matumaini hata CCM watawasilisha majibu yao kwa Ofisi ya Msajili hivyo tunaendelea kuipongeza ofisi hiyo kwa sababu haijaogopa kuchukua hatua kwa taasisi yoyote ya kisiasa,”.
Pia ameitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kuchukua hatua kwa vyama au viongozi watakaobainika kwenda kinyume na sheria bila kuangalia ukubwa wa chama husika au ushawishi wake wa kisiasa.

Kwa mujibu wa Doyo, taasisi yoyote inayosimamia sheria inaposhindwa kutekeleza wajibu wake kwa wakati, hujenga mazingira ya sintofahamu, migogoro na kuporomoka kwa nidhamu ya kisiasa nchini.
“Tutakapokuwa na taasisi ambayo haina uwezo wa kushughulikia matatizo ya jambo inalolisimamia, kitakachokuja ni maafa na uvunjifu wa amani,ndiyo maana tumejitokeza mbele ya Watanzania kueleza kuwa kila upande unapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria,”amesema Doyo.

More Stories
Watuhumiwa kulima bangi zaidi ya ekari 10
MNEC Mwaselela: Samia ana dhamira kwa vijana
Elimu ya kijinsia yatolewa Tandale Yemeni