March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia:Serikali ya awamu ya sita imefanya makubwa Kata ya Mwasanga

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo jipya la Uyole, Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya maendeleo makubwa katika kata ya Mwasanga, hususan kwenye sekta ya elimu na miundombinu.

Akizungumza Septemba 12, 2025, katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea udiwani wa CCM kata ya Mwasanga, Brandy Nelson, uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwasanga, Dkt. Tulia alisema changamoto ya uhaba wa madawati katika shule za msingi na sekondari imepatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Hivi sasa hakuna mwanafunzi anayekaa chini kwa kukosa dawati. Tatizo la madawati halipo tena. Serikali ya awamu ya sita imeshughulikia mahitaji muhimu ya shule na hakuna mzazi anayechangishwa fedha kwa ajili ya madawati,” amesema Dkt. Tulia.

Kuhusu miundombinu ya barabara, Dkt. Tulia alisema serikali imepanga kuweka lami katika mitaa ya Mwasanga ambayo kwa sasa inakabiliwa na vumbi na changamoto za usafiri. Alisema hatua hiyo itasaidia hasa akina mama wafanyabiashara wadogo wanaouza mboga katika maeneo ya milima ya Insoso.

“Tumethibitisha kuwa tunaweza, mfano ni ujenzi wa daraja tuliloahidi na sasa limekamilika. Hivyo basi, muwe na imani nasi kwa kumchagua Brandy Nelson kuwa diwani wenu pamoja na kuendelea kumuunga mkono Rais Samia ili utekelezaji wa miradi iendelee kwa kasi,” amesisitiza Dkt.Tulia.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa kata hiyo, Brandy Nelson, ameshukuru Dkt. Tulia kwa mchango mkubwa alioutoa katika maendeleo ya Mwasanga, akitaja ujenzi wa daraja lililokuwa chanzo cha ajali na vifo vya wananchi.

“Daraja hili lilichukua maisha ya baadhi ya wananchi na watoto wadogo. Serikali ilitoa zaidi ya shilingi bilioni moja kujenga daraja hili baada ya jitihada za Dkt. Tulia. Sasa jukumu letu ni kuhakikisha Oktoba tunampatia kura za kishindo Rais Samia na Dkt. Tulia,” amesema Nelson.

Wananchi nao walieleza imani yao kwa mgombea huyo. Mage Mwankenja, mkazi wa Mwasanga, alisema Nelson amekuwa kiongozi wa kujitoa kwa wananchi tangu akiwa mjumbe wa serikali ya mtaa kwa miaka sita, ambapo alionyesha jitihada kubwa za kuleta maendeleo.

Naye mwenyekiti wa mtaa wa Nduye, Furaha Saimon, amesema Nelson ni kiongozi mnyenyekevu, mwadilifu na mwenye dhamira ya kweli ya kuendeleza kata hiyo katika kutatua changamoto mbalimbali.

“Kwa kumchagua Brandy Nelson, tunaamini kata ya Mwasanga itapiga hatua kubwa kimaendeleo na kufungua fursa mpya kwa wananchi wake,”amesema.