April 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya,Helen Keller kuendesha kambi ya macho Songwe

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Helen Keller, wameandaa kambi ya siku sita ya upasuaji wa mtoto wa jicho itakayofanyika katika Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 19, 2025 ambapo zaidi ya wananchi 700 wanatarajiwa kunufaika na huduma hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 12, 2025, Mratibu wa Huduma za Macho Mkoa wa Songwe, Dkt.Jofrey Josephati, amesema kambi hiyo imelenga kupunguza kasi ya ongezeko la wagonjwa wa mtoto wa jicho, hususan vijijini ambako huduma hizo ni ngumu kupatikana.

“Tumeamua kusogeza huduma hizi adimu karibu na wananchi ili kupunguza tatizo la upofu unaoweza kuzuilika. Kupitia kambi hii, wananchi watapata matibabu ya macho bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali kubwa,” amesema Dkt. Josephati.

Ameongeza kuwa ugonjwa wa mtoto wa jicho husababishwa na mambo mbalimbali ikiwamo kuzeeka, mtindo wa maisha, kisukari, na matumizi ya muda mrefu ya dawa za steroid.

Kwa upande wake, Dkt. Barnabas Mshangila, Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, alisema upasuaji huo huchukua muda mfupi na mgonjwa hutolewa dawa za kupunguza maumivu, hivyo hana maumivu makali.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji, mara nyingi mgonjwa huanza kuona tena ndani ya siku moja, hali inayorejesha matumaini na uwezo wa kushiriki shughuli za kila siku,” amesema Dkt. Mshangila.

Naye Meneja Mradi wa Shirika la Helen Keller, Athumani Tawakali, alisema shirika hilo linaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha huduma za macho nchini. Alishukuru Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Serikali ya Mkoa wa Songwe kwa ushirikiano wao.

“Mradi huu, unaofadhiliwa na Alcon Foundation, unalenga kurejesha nuru kwa maelfu ya wananchi katika mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa,” alisema Tawakali.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma, akiwamo Edward Mkoko na Ericka Mziho, waliishukuru serikali, madaktari bingwa na waandaaji wa kambi hiyo kwa kuwasogezea huduma bila gharama yoyote.