May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia,Madiwani kushirikiana kuboresha miundombinu ya elimu

Na Esther Macha,Timesmajira Online,Mbeya

MADIWANI wa halmashauri ya jiji la Mbeya Kwa kushirikiana na ofisi ya Mbunge wamekuja na mkakati wa kuboresha miundombinu ya elimu Katika shule za msingi na sekondari ili ziendane na jiji hilo.

Halmashauri ya jiji la Mbeya ina jumla ya Kata 36, lakini imekuwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya elimu kutokana na shule nyingi kuwa za zamani hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya sasa.

Akizungumza na wakazi wa mtaa wa Nonde, jijini hapa kabla ya kumkabidhi nyumba aliyomjengea ,mzee Aswile Mwakigege, Mbunge wa jimbo la Mbeya mjini  Spika wa Bunge  Dk.Tulia Ackson amesema dhamira yao ni kuondoa changamoto za elimu.

Dk.Tulia ambaye pia ni spika wa Bunge na Rais wa mabunge duniani (IPU) amesema sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto nyingi hasa za miundombinu lakini serikali ya awamu ya sita imefanya kila linalowezekana ili kuhakikisha inatatua changamoto hizo.

“Wote tumeona namna serikali yetu inavyopambana, mstahiki Meya ameeleza ile program ya kukamilisha matundu yote ya vyoo Kwa shule za msingi Hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu,”amesema.

Amesema Katika mipango yao shule zote za mjini ni lazima zibadilishwe kutoka miundombinu ya zamani kuwa ya kisasa itakayoendana na hadhi ya Jiji.

Pia changamoto za matundu ya vyoo inaenda kuwa historia, madawati na idadi ya walimu itakuwa ya kujitosheleza lengo likiwa ni kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia.

Naye Meya wa Jiji la Mbeya,Dour Issah Mohamef  amesema kulikuwa na upungufu wa matundu 509 ya vyoo lakini kwa muda mfupi serikali imejenga matundu 310 na kwamba yaliyosalia yatakamilishwa hivi karibuni.

Amesema Katika program ya shule kuendana na hadhi ya jiji kuanzia mwezi Mei wataanza kujenga vyumba 20 vya madarasa kila mwezi.