Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson ametoa wito kwa jamii kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ili kuipunguzia mzigo serikali wa magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt.Tulia ametoa wito huo jijini hapa leo,Aprili 13,2024,uwanja wa Jamhuri wakati akizungumza baada ya mbio za Bunge Marathon zilizofanyika kwa lengo lakukusanya fedha kwa ajili ya kujenga Shule ya Sekondari ya Wavulana.
Amesema kuwa licha ya Bunge kuja na wazo la marathoni hiyo kwa lengo la kujenga shule lakini Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kupambana na magonjwa hayo,hivyo jamii inapaswa kuthamini michezo.
“Nimefurahishwa na mzee wa Miaka 91 kukimbia mbio za kilomita 10 na watoto kuanzia umri wa miaka 5 hadi 11 kukimbia mbio za kilomita 5 na nimemuona na mlemavu pia amekimbia kwa kiti naye tutampa zawadi hongereni Sana kwa kujitoa kwenu kwani hivi ndivyo tunatakiwa kuwa,”amesema
“Tunawashukuru watu wote walioshiriki na niwambie tu kwa kutambua mchango wenu kila mchangiaji jina lake litaandikwa kwa wino wa dhahabu na kihifadhiwa katika shule hiyo siku yoyote ukitembelea pale utaona jina lako,”amesema Dkt.Tulia.
Mbio hizo za kuanzia Km 21, Km 10 na Km 5 zimeongozwa na wadau mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya, Wabunge na Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi pamoja na wadau wa michezo baada ya kumalizika washindi walipewa zawadi zao.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa