May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Denmark yampongeza Samia kwa mafanikio ya kiuchumi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

SERIKALI Denmark imempongeza
Rais Samia Suluhu Hassan,kwa hatua
kubwa ambayo nchi imepiga kiuchumi,
licha ya ulimwengu kukabiliwa na
changamoto mbalimbali na kwamba
anaiona Tanzania kuwa moja ya nchi
kubwa kiuchumi kwa siku zijazo.

Hayo yamesemwa Wa ziri wa
Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za
Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark,
Dan J√∏rgesen, jijini Dodoma mwishoni
mwa wiki wakati akizungumza na Waziri
wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

Aliishauri Tanzania, kuishauri Denmark
namna ya kuboresha ushirikiano na
maeneo ya kimkakati ambayo nchi
inataka kuyapa kipaumbele hususan
katika eneo la uwekezaji na biashara
katika mpango wake mpya wa ushirikiano
na nchi za Afrika ambao nchi yake
inauandaa na wanatarajia utazinduliwa
na Rais Samia ambaye amealikwa
kuitembelea nchi hiyo.

Kwa upande wake Waziri Dkt.
Nchemba ameihakikishia Denmark
kwamba Tanzania iko tayari kushirikiana
na nchi hiyo kupitia Mkakati wake
mpya wa ushirikiano wa kimataifa kwa
kuishirikisha sekta binafsi katika mipango
yake ya maendeleo ili kukuza uchumi
na ajira.

Dkt. Nchemba aliyasema hayo
alipokutana na kufanya mazungumzo
na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo
na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa
Denmark, Dan J√∏rgesen, jijini Dodoma.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania
ina fursa kubwa za uwekezaji katika sekta
mbalimbali na kutoa wito kwa kampuni,
mashirika na Taasisi mbalimbali kutoka
Denmark kushirikiana na sekta binafsi ya
Tanzania kuwekeza mitaji na teknolojia
ili pande zote mbili ziwezeze kunufaika.

Alisema kuwa mkazo mkubwa wa
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa
na Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni
kuhakikisha kuwa Sekta binafsi ndiyo
inayotakiwa kuendesha uchumi wa nchi
na kwamba ili kufanikisha mpango huo,
Serikali imefanya mageuzi makubwa ya
kisera na kisheria ili kuboresha mazingira
ya uwekezaji nchini.

Dkt. Nchemba aliyataja baadhi ya
maeneo yanayohitaji ushiriki wa sekta
binafsi kuwa ni pamoja na uendeshaji
wa reli ya kisasa ya SGR, masuala ya
nishati, kilimo, na maeneo mengine kadha
wa kadha.

Alisema kuwa Tanzania iko tayari
kushirikiana na Denmark kupitia mpango
wake mpya wa ushirikiano baada ya
kusitisha uamuzi huo wa kufunga ubalozi
wake nchini ambapo nchi hiyo imepanga
kuongeza kiwango cha ufadhili na
kuelekeza fedha hizo kwenye maeneo
yatakayokuza uchumi, ikiwemo nishati,
kuboresha mifumo ya kodi, kilimo, elimu,
afya, pamoja na kusaidia sekta binafsi.

Dkt. Nchemba alirejea shukrani zake
kwa Denmark kwa kuendeleza ushirikiano
wake uliotimiza miaka 60, ambapo
katika miaka ya hivi karibuni, nchi hizo
mbili zilikuwa zikitekeleza miradi ambayo
Denmark iliipatia Tanzania msaada wa
takriban Denish Krone bilioni 2, sawa na
shilingi za Tanzania bilioni 646.

Aidha, alisema kuwa Denmark
kupitia Shirika lake la Maendeleo
(DANIDA), imetoa zaidi ya sh. bilioni
103 zinazotokana na mapato ya uwekezaji
wake wa hisa katika Benki ya CRDB,
ambazo zimetumika kwa ajili ya kusaidia
sekta ya afya kupitia Mfuko wa Afya.

Aliiomba pia Denmark kupitia Taasisi
yake inayohusika na masuala ya Bima
na Dhamana (Danish Export Credit
Agency), kushiriki katika ujenzi wa
mradi wa SGR kwa vipande vilivyobaki
kutokana na umuhimu wa mradi huo
katika kukuza biashara na ustawi wa
maisha ya watu watakao tumia reli hiyo
pamoja na kukuza pato la Taifa.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na
Naibu Waziri wa Maendeleo wa Serikali
ya Denmark, Mhe. Lotte Machon,
Balozi wa Denmark nchini Tanzania,
Mette Dissing-Spandet, Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry
Mwamba, Balozi wa Tanzania katika
nchi za Scandinavia, Dkt. Grace Olotu,
na Balozi wa Tanzania wa Heshima
nchini Denmark, Mhe. Simon Mears
na Viongozi wengine waandamizi wa
Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na
Serikali ya Denmark.